0

TBS YAVUNA BIL 1.5/UKAGUZI WA MAGARI NCHINI

60ae424dcaf319af88d3458f0c16a6cc.jpeg TBS YAVUNA BIL 1.5/UKAGUZI WA MAGARI NCHINI

Thu, 10 Jun 2021 Source: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imeingiza Sh bilioni 1.5 katika kipindi cha wiki tangu tangu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lianze ukaguzi wa ubora wa magari yaliyotumika yanayotoka nje ya nchi na kuingia nchini.

Fedha hizo zimeingia kutokana na ukaguzi uliofanyika kati ya Aprili 15 mwaka huu hadi Mei 8, mwaka huu kwa ukaguzi wa magari 4,779.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Mafunzo kwa wahariri wa vyombo vya habari jana Dar es Salaam juu ya majukumu ya TBS, Meneja wa Ukaguzi wa Bidhaa zinazotoka Nje, Said Mkwawa alisema kati ya magari hayo 4,779 yaliyokaguliwa, magari 3,445 hayakuwa na dosari yoyote.

“Magari 1,334 yalikuwa na dosari na tuliwaelekeza wamiliki wakafanye marekebisho. Asilimia 85 ya magari yote tuliyokagua tumekuta yana dosari katika taa, magurudumu, kashata za magurudumu zimeisha, kiujumla matatizo yake si makubwa,” alisema Mkwama.

TBS katika ukaguzi wake kwenye magari yanayoingia nchini kutoka nje inaangalia mionzi, ubora wa magurudumu, moshi wa exhaust, breki, mngurumo wa gari na ubora wa gari kijumla.

Kabla ya TBS kuanza ukaguzi huo Aprili 15, mwaka huu, kazi hiyo ilikuwa ikifanywa nje ya nchi magari yanapotokea.

Gharama za kufanya ukaguzi huo kwa nchini ni Sh 350,000 na malipo yanafanyika kwa njia ya kielektroniki bila kuongeza wala kupunguza kiwango cha fedha. Sehemu kubwa kubwa ya magari yanayoingia nchini yanatokea Japan ikifuatiwa na nchi za Urabuni na sehemu ndogo Ulaya.

Mkwawa alisema kuanzia mwezi huu magari mengi zaidi yatakaguliwa nchini kwa sababu mengi hayatakuwa na vyeti vinavyoonesha yalikaguliwa nje. Wakati wanaanza ukaguzi huu nchini magari

mengi yalikuwa yameshapimwa kwenye nchi yanapotoka na kupewa vyeti vya kutibitisha ukaguzi huo.

Naye Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS, Diocles Ntamulyango alisema kituo chao cha kupimia magari hayo cha bandarini kina uwezo wa kupima magari 384 kwa siku na kituo cha UDA uwezo wake ni kupima magari 96 kwa siku.

Alisema katika kuboresha upimaji, wameshaagiza mitambo mingine 12 yenye uwezo wa kupima magari 1,200 kwa siku. Mitambo hiyo iliyoagizwa Ujerumani kwa gharama ya Sh bilioni tatu inatarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz