0

Samia: Hatukubahatisha kufika uchumi wa kati

Samia: Hatukubahatisha kufika uchumi wa kati

Mon, 19 Oct 2020 Source: HabariLeo

SEKTA binafsi kupitia wafanyabiashara wadogo na wakubwa wamefanya kongamano kumpongeza Rais John Magufuli na serikali ya Awamu ya Tano kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano.

Wafanyabiashara hao walipongeza namna ambavyo serikali hiyo ilivyoiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati bila kubahatisha, kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kupambana kikamilifu na ugonjwa wa corona lakini pia kudhibiti rushwa kandamizi husuani kwa wafanyabiashara wadogo.

Akizungumza katika kongamano hilo, lililohudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula alisema ndani ya kipindi cha miaka mitano Rais huyo amefanya mambo mengi makubwa yatakayoipaisha Tanzania kiuchumi.

“Nampongeza kwa kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati. Kwa baadhi ya wasiofahamu wanaweza kufikiri tumefikia uchumi wa kati kwa kubahatisha lakini kazi kubwa imefanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na kufikia mapema zaidi kuliko ilivyotarajiwa,” alisema Ngalula.

Alisema pia TPSF inampongeza Rais Magufuli kwa namna alivyoshughulikia suala la covid 19, na mpaka sasa kuna nchi bado ziko kwenye wakati mgumu kiuchumi.

Alisema kabla ya ugonjwa huo uchumi wa Afrika ulitarajiwa kukua kwa asilimia 3.2 lakini kutokana na janga hilo la uchumi wa Afrika matarajio yalirudi kwenye asilimia hasi 0.8 wakati Tanzania bado ina matarajio ya uchumi wake kukua kwa asilimia 5.9.

“Kenya waliokwenda kwenye lockdown walitarajia uchumi wao kukua kwa asilimia 5.9 lakini sasa wanatarajiwa kukua kwa asilimia moja. Na si Kenya nchi kama Afrika Kusini na Ethiopia nazo uchumi wake umeshuka.Hii ndio tofauti kubwa na Tanzania,” alisema Ngalula na kuongeza;

“Tumempata Rais shupavu aliyechukua maamuzi sahihi kwa mustakabali wa biashara zetu leo wengi tungefunga maduka, biashara na mikopo tungeshindwa hata kulipa,”

Alimpongeza Dk Magufuli kutokana na uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye miundombinu ya barabara, madaraja na barabara za juu.

“Wengi tunafahamu ilikuwa inachukua saa nane kutoka Bandari ya Dar es salaam kufika check point Misugusugu, saa zote hizo zilikuwa zinapotea makutano ya Ubungo,” alisema Ngalula.

Alisema kwa sasa kutoka bandari hiyo hadi Misugusugu hata saa mbili hazifiki.

“Faida haikuwa kwa wakazi wa Dar es Salaam pekee inakwenda mpaka kwa mkulima wa chini. Mfano kusafirisha tani moja ya mbolea kutoka China kuja Tanzania haizidi Sh 100,000 lakini kutokana na ucheleweshaji ilikuwa kutoka Dar es Salaam hadi Tabora ni zaidi ya Sh 200,000”alisema.

Ngalula alimpongeza Magufuli kwa kufufua na kuwekeza katika Shirika la Ndege la ATCL, na hivyo kufanikisha kutimiza maono ya Dk Magufuli ya kuitengeneza Tanzania kuwa kituo cha biashara.

“Hakuna jinsi yeyote unaweza kutengeneza hub ya kibiashara kama hauna ndege. Ni rahisi kufungua biashara Dubai kwa sababu ya ndege nyingi nchi kama Uingereza wanafungua ofisi Kenya au Afrika Kusini kwa sababu ya usafiri wa anga,” alieleza.

Kwa upande wa rushwa, alisema Serikali ya Awamu ya tano, imefanya kazi kubwa ya kudhibiti tatizo hilo ambalo lilikuwa kero kubwa hususani kwa wafanyabiashara wadogo.

Alisema kipindi cha nyuma wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakinunua bidhaa kutoka China sawa na wafanyabiashara wakubwa walikutana na adha kubwa ya kuharibiwa mizigo yao na wengi walijikuta mitaji yao ikikata.

“ Ukileta biashara na mfanyabiashara mkubwa ikifika bandarini kontena halitoki kunakuwa na visingizo mara bidhaa hazina kiwango au TBS wanateketeza kwa sababu ya rushwa. Mfanyabiashara mshindani wako anakwenda kutoa rushwa na mzigo wako unakamatwa lakini vitu hivyo sasa vimekwisha” alisisitiza.

Mwenyekiti wa Vibindo Society, Gaston Kikui alimshukuru Dk Magufuli kwa kuanzisha vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo sasa vimekuwa mkombozi kwa wajasirimali wengi, ikiwemo kuwapatia mikopo nafuu.

“Tulikuwa tunapata shida sana wenye mitaji midogo iliikia mahali tunakodi watu wa bodaboda, ili aende pale jiji achungulie gari la jiji linatoka saa ngapi na linaelekea wapi na kupigiana simu kuondoka maeneo linakoelekea, lakini sasa hili tumeondokana nalo, ttunamuombea sana Rais wetu,” alisema

Alisema pia anamshukuru rais kwa kutoa Sh milioni 25 kwa ajili ya kusaidia wajasiriamali wa pale feri zikiwemo Sh milioni tano kwa ajili ya mama lishe.

“Sisi kama vibindo tuna kura milioni tatu na nusu kutoka kwetu hiyo haina mjadala nyongeza tunakuhakikishia, Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya, Iringa na Dodoma,” alisitiza.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Machinga Tanzania, Steven Lusinde alisema Rais Magufuli amewatoa utumwani na kuwapeleka wamachinga katika nchi ya ahadi.

“Bodaboda, mama lishe na machinga baba na mama ni mmoja. Tumetembea mikoa 16 tukihamasisha mama lishe, bodaboda na machinga kuhakikisha tunafuata sheria na kupata kitambulisho cha ujasiriamali na kuwa na bima za afya,”alisema na kuongeza;

“Na mimi kama Makamu Mwenyekiti sizungumzii hadithi ukitaka uhondo wa ngoma uingie ucheze, kuna watu wanazungumza vitu hata hawavijui, leo hii mike (kinasa sauti) mmachinga ninapata fursa ya kuitumia na wafanyabiashara wengine wakubwa humu ndani haijawahi kutokea ndani ya taifa hili,”

Lusinde alielezea faida ya vitambulisho vya wajasiriamali ikiwa ni pamoja na kupata mikopo rahisi ambayo aliita kama kuazimwa na si kukopewa.

Alisema kuitia benki mbalimbali mmachinga kwa kutumia kitambulisho hicho cha ujasiriamali anaweza kukopeshwa kuanzia Sh 200,000 hadi 500,000 kwa riba ya Sh 2,000.

Mwakilishi wa sekta ya nishaji Ngwisa Mpembe alisema tangu mwaka 2015 serikali ilipoingia madarakani, kumekuwa na mchango mkubwa wa sekta binafsi kwenye eneo la nishati. Jumla ya vijiji 9,000 kati ya 12,000 vina umeme wa uhakika

Mwakilishi wa sekta ya Ujenzi Baru Jog alimshukuru serikali kwa kutekeleza miradi mingi ya ujenzi kama vile miundombinu kama vile barabara, madaraja, vivuko na ujenzi wa SGR na upanuzi wa bandari.

Alimshukuru Rais kwa kuongeza vigezo vya ushiriki kwa wakandarasi wazawa na kuweka kiwango cha Sh bilioni 10 kwa miradi kwa ajili ya wakandarasi wa ndani.

“Hatujawahi kupewa kipaumbele kama hiki. Pia tuna kupongeza kuwezesha kampuni za wakandarasi wa ndani kushiriki katika miradi mikubwa kama ujenzi wa umeme wa Mwalimu Nyrerere. Tunakuhitaji kwa miaka mitano zaidi ili utusaidia zaidi na n chi yetu kwa ujumla,” alisema.

Wengine waliotoa shukrani zao na kuelezea mafanikio waliyopata kutokana na mchango wa serikali ni pamoja na mama lishe, baba lishe, bodaboda, kampuni za mawasiliano, wafanyabiashara wasindikaji, taasisi za fedha na sekta za mafuta na gesi.

Chanzo: HabariLeo