0

NMB yasifiwa kwa kuokoa maisha

NMB yasifiwa kwa kuokoa maisha

Thu, 8 Apr 2021 Source: HabariLeo

WATUMISHI wa afya mkoani Kilimanjaro wameisifu Benki ya NMB kwa kuchangia kuokoa maisha kwa kutoa misaada katika vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.

Misaada hiyo imewezesha kuboreshwa kwa huduma za afya na hivyo kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika.

Misaada hiyo ni sehemu ya mpango wa uwajibikaji katika jamii (CSR) wenye bajeti ya takribani Sh bilioni moja kwa mwaka.

Wiki hii, benki hiyo ilitoa misaada katika kanda yao ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha, kwa kutembelea vituo vinne vya afya kikiwemo kituo cha afya kilichopo katika Chuo cha Polisi (CCP) Moshi, Kituo cha Afya Pasua wilayani Moshi, Hospitali ya Wilaya Hai na Kituo cha Afya Oltrumet wilayani Arusha.

Katika Kituo cha Afya Pasua, Benki ya NMB imesaidia vitanda na vifaa vya kujifungulia ambako Ofisa Muuguzi Msaidizi, Mwantumu Silayo alitoa ushuhuda namna walivyopiga hatua baada ya kupokea msaada huo.

“Hakika tulikuwa na changamoto kubwa ya vitanda vya uchunguzi na vya kulalia wagonjwa wodini. Kutoka NMB tumepokea vitanda vya kufanyia uchunguzi viwili, vitanda vya kulalia wagonjwa vitano, shuka 49 na vifaa vya kuzalishia wajawazito,” alieleza Silayo.

Aliongeza, “Kwa mwezi tunapokea zaidi ya wagonjwa 150. Awali daktari alikuwa analazimika kumfanyia uchunguzi mgonjwa huku amesimama au amekaa kwenye kiti. Kimsingi mgonjwa anatakiwa alale hasa kwa wajawazito au watu wenye matatizo kwenye via vya uzazi. Kwa sasa mambo ni mazuri na hata idadi ya wajawazito wanaojifungua imeongezeka.”

Mwakilishi wa Hospitali ya Oltrumet wilayani Arusha, Dk Consolata Sweya alisema wamepokea magodoro, shuka na vitanda vya kulalia wagonjwa.

“Msaada huu umerudisha uhai wa hospitali yetu, ndiyo maana vitanda vyote tuliamua kuvipeleka wodi ya wazazi. Hospitali hii awali ilisahauliwa, lakini katika uongozi wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alipotembelea hapa akaagiza ifufuliwe. Kwa sasa inahudumia eneo kubwa ni kama hospitali ya wilaya vile,” alisema Dk Sweya.

“Kwa siku tunazalisha kati ya wajawazito kumi hadi 13, wodi ya wazazi ina vitanda 18. Lakini changamoto kubwa tuliyonayo ni vitanda vya watoto njiti. Hivyo tunaiomba NMB itufikirie katika eneo la watoto njiti,” aliongeza.

Kwa upande wake, Ofisa Uwajibikaji kwa Jamii wa NMB, Aloyce Kikois alisema, “Katika utekelezaji wa wajibu wetu kwa jamii, tumejikita zaidi katika maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni elimu, afya na huduma jumuishi za fedha na huwa tunatenga asilimia moja ya faida ya benki baada ya kodi kwa ajili hiyo. Kila tunachokifanya huwa tunalenga kuhakikisha kinaongeza thamani kwenye jamii husika na kuonesha uendelevu wa malengo yetu.”

Kwenye upande wa afya, Kikois alisema lengo kuu ni kuhakikisha vifaa tiba vipo kwa ajili ya wateja wao, wadau na jamii kwa ujumla kwa kutoa vitanda vya wodini, vitanda vya kujifungulia na vifaa vingine muhimu kwa utabibu.

Alisema NMB iliamua kuchagua afya kama moja ya sekta ambazo zitapokea msaada kutokana na benki hiyo kuthamini umuhimu wa wajawazito, watoto na watu wengine wanaohudumiwa kwenye vituo hivyo na Watanzania wote kwa ujumla.

“Tunataka wateja wetu wawe na uhakika wa afya zao. Mwaka mzima tunafanya nao biashara wakiwa na afya njema, lakini wanapougua lazima wajue sisi pia tupo kwa ajili yao. Ndiyo maana tumeamua kati ya faida inayopatikana na sekta ya afya nayo ifaidike,” alisema Kikois wakati wa ziara hiyo.

Katika ziara hiyo ya kukutana na wanufaika wa uwekezaji wa NMB wa CSR na kutathimini matokeo yake, maofisa hao pia walitembelea shule za msingi na sekondari ambazo pia zilizopokea misaada katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

NMB imekuwa kinara wa kuwekeza katika miradi ya kijamii kutokana na ufanisi wa shughuli zake ikiwemo kuongoza kutengeneza faida ambayo huiwezesha kutenga kiasi kikubwa cha fedha ikitumia zaidi ya Sh bilioni tano kati ya mwaka 2015 na 2020 kwa ajili ya kurejesha faida kwa jamii.

Chanzo: HabariLeo