0

NBAA yataka mafunzo wahasibu wanawake

NBAA yataka mafunzo wahasibu wanawake

Thu, 12 Nov 2020 Source: HabariLeo

BODI ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa Taifa (NBAA), imezitaka taasisi mbalimbali nchini kutoa kipaumbele cha mafunzo kwa wahasibu wanawake waliopo katika taasisi hizo ili kuwajengea uwezo zaidi kutekeleza majukumu yao.

Mkurugenzi Mkuu wa NBAA, Pius Maneno, alitoa rai hiyo juzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wahasibu Duniani iliyoandaliwa na Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) na kuwashirikisha wahasibu kutoka taasisi mbalimbali nchini. Alisema kuna kila sababu kwa taasisi hizo kutoa kipaumbele kwa wahasibu wanawake kutokana na umuhimu wao katika kuiendeleza kazi ya uhasibu nchini.

Maneno alisema ni vyema pia kwa kundi hilo kuongeza juhudi ya kuzishauri taasisi zao katika masuala ya kihasibu ili kuziongezea tija.

"Wahasibu wanawake wanafanya mambo mengi sana, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha wajasiriamali wadogo mitaani, hivyo ni vyema tukazidi kuwaunga mkono ili kuiendeleza fani ya uhasibu nchini," alisema.

Aidha alisema NBAA kwa kushirikiana na TAWCA imekuwa mstari wa mbele kuwajengea uwezo wanawake waliopo katika vyuo na taasisi mbalimbali nchini ili kuongeza idadi ya wahasibu wanawake.

Alisema hatua hiyo inasababishwa na uchache wao kwani miongoni mwa wahasibu 10,500 waliopo nchini, wahasibu wanawake ni 3,000 hali inayoibua haja ya kufanya kila linalowezekana kuongeza idadi hiyo.

Mwenyekiti wa TAWCA, Neema Mssusa, aliwataka wahasibu wote kutoka nje ya nyumbani na ofisi zao na badala yake, waende katika taasisi mbalimbali kufanya kazi za kihasibu au kuzishauri menejimenti husika ili kuleta ufanisi wa fani hiyo.

Alisema kitendo cha baadhi ya wahasibu kujifungia ndani siyo kizuri kwa kuwa kinawanyima fursa ya kuonesha uwezo wao.

Chanzo: HabariLeo