0

Mapato ya uvuvi  Mkinga yafikia mil. 97/-

Mapato ya uvuvi Mkinga yafikia mil. 97/-

Mon, 5 Oct 2020 Source: HabariLeo

MAPATO ya Halmashauri ya Mkinga mkoani Tanga kupitia sekta ya uvuvi yamepanda kufikia Sh milioni 96.6 mwaka 2019/ 2020

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga, Rashid Gembe amesema mapato hayo yamepanda kutokana na mikakati waliyoiweka dhidi ya uvuvi haramu.

Alibainisha hayo wakati akizungumza na timu ya wataalamu kutoka Mradi wa Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOfish) ofisini kwake mwishoni mwa wiki.

Alisema mwaka 2015/ 2016 kabla ya mradi huo kuanza kuhamasisha uvuvi endelevu na wenye tija, Halmashauri ya Mkinga ilikusanya Sh milioni 45.3 kutoka katika sekta ya uvuvi.

Gembe aliwaeleza wataalamu hao wanaofuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wilayani humo kuwa mradi huo umekomesha uvuvi haramu hususani uvuvi wa kutumia mabomu na makokoro.

“Mradi wa SWIOfish ulipoanza kufanya kazi wilayani kwetu mwaka 2016 ulianzisha Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari (BMU) vipatavo 14 ambavyo vimekuwa vikitoa elimu ya ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwa wananchi ikiwemo kutunza mazingira ya fukwe za bahari,”alisema na kuongeza:

“Pia mradi uliimarisha doria za baharini na nchi kavu kwa lengo la kulinda rasilimali za uvuvi, doria hizo zimepunguza uvuvi haramu na sasa mapato ya halmashauri yameanza kupanda kwa sababu wavuvi sasa wanafanya uvunaji endelevu wa rasilimali za uvuvi”.

Aliwakumbusha wananchi kuwa mapambano dhidi ya uvuvi haramu, sio nguvu ya soda bali ni mapambano endelevu na hawatakuwa na huruma na yeyote atakayekwenda kinyume.

Chanzo: HabariLeo