0

Mapato ya maliasili, utalii kuongezeka

Mapato ya maliasili, utalii kuongezeka

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeweka mikakati ya kuimarisha utalii na uwindaji wa wanyamapori ili kuongeza mapato katika uchumi wa taifa katika miaka mitano ijayo.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Aloyce Nzuki alisema hayo kwenye hotuba yake jana kwa viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) katika kikao cha siku tatu kilichofanyika mjini hapa.

Dk Nzuki aliiitaka Tawa kufikia malengo ya serikali kuhusu utalii wa uwindaji ifikapo mwaka 2025/2026.

Alieleza kuwa katika kuhakikisha kuwa mapato ya nchi yanaongezeka, Ilani ya CCM ya mwaka 2021/2022- 2025/2026 imeielekeza wizara kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza na kukuza wigo wa bidhaa na mazao ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,510,151 mwaka 2019/2020 hadi watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025/ 2026.

Alisema moja ya mapato yatokanayo na utalii, yanatakiwa kuongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2020 hadi dola za Marekani bilioni sita mwaka 2025/2026.

"Ili kufikia malengo hayo, wizara inaelekeza Tawa kukuza na kuimarisha utalii wa picha na uwindaji katika mapori ya akiba , mapori tengefu na maeneo ya wazi kuendeleza maeneo ya malikale ya Kilwa na Kunduchi na kuyatumia kwa utalii wa fukwe,"alisema.

Katika kutanua masoko ya uwindaji wa kitalii, Katibu Mkuu huyo aliiagiza Tawa kuandaa andiko kwa ajili ya kutangaza uwindaji wa kitalii katika masoko mbalimbali duniani mfano Urusi, Ukraine , Asia ya Kati, Brazil na Australia.

"Andiko hilo litumike kutengeneza video ambayo itapelekwa kwa mabalozi wa Tanzania waliopo nchi mbalimbali ili wasaidie kutangaza uwindaji wa kitalii,"alisema.

Kutokana na umuhimu wa suala hilo, Nzuki alitoa mwezi mmoja kwa Tawa kukamilisha kazi hiyo. Alitaka ifikapo Desemba 15 mwaka huu mikutano ya mtandao kwa madhumini hayo iwe imeanza.

Kaimu Kamishna wa Tawa, Mabula Nyanda alisema mamlaka imechukua hatua mbalimbali, kukabiliana na watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na ujangili, mfano kutoa elimu.

Alisema katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, elimu imetolewa kwa watumishi 351 katika vituo 15 vya mamlaka. Elimu hiyo inatolewa na Tawa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Chanzo: HabariLeo