0

Wachimbaji wataka mitaji kuwekeza madini ya viwanda

Mon, 22 Feb 2021 Source: habarileo.co.tz

WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini wameiomba serikali iwawezeshe mitaji ya vifaa ili wawekeze kwenye uchimbaji wa madini ya viwanda.

Walitaja madini hayo kuwa ni pamoja na mchanga, jasi, ulanga, chuma, kokoto, makaa ya mawe, magadi, kinywe (graphite), kaolin lakini pia iwatafutie soko la uhakika wa madini hayo.

Waliyabainisha hayo jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania 2021 ulioanza jana. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuufungua leo.

Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya, alisema mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano alioufanya Rais John Magufuli mwaka 2019 alipokutana na wachimbaji wadogo ambao walieleza changamoto mbalimbali walizokabiliana nazo ambazo serikali ilizipatia ufumbuzi kwa kiasi kikubwa.

Profesa Manya alisema mkutano huo pia unatoa fursa kwa serikali na wachimbaji hao kuendelea kujadiliana kwa lengo la kuboresha sekta ya madini kwa faida ya pande zote mbili.

Wakati wa majadiliano yaliyoongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe, Serikali imewataka wachimbaji wadogo kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini ya viwanda kwani nayo ni fursa kubwa na muhimu katika kuwainua kiuchumi lakini pia kuchangia Pato la Taifa.

Mchimbaji Mdogo wa madini ya ujenzi na viwanda kutoka Mkoa wa Dodoma, Rodgers Sezero, alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa mitaji ya vifaa kama vile mashine nzito za kuchimbia, mashine za kuchoronga miamba na malori ya kubebea madini hayo.

“Mimi nachimba madini ya ujenzi na viwanda kikiwemo chuma, kifusi, mchanga, copper na nickel, kwa hiyo naiomba Serikali itukopeshe mitaji ya vifaa na siyo fedha, mimi kwa mfano nahitaji excavator nne, malori, ambayo nikipata nitafanya uwekezaji mkubwa, nitatengeneza ajira na serikali itapata mapato,”alisema Sezero.

Mchimbaji mwingine wa madini ya viwanda, Sarah Msambagula, aliiomba serikali iwapatie taarifa za utafiti wa madini ya viwanda ili wajue urefu na upana wa miamba ya madini hiyo, wapatiwe vibali vya kuuza nje sehemu ya madini ya viwanda kwa kuwa soko la ndani ni dogo, wanahitaji mitambo mikubwa ya kuchimbia, umeme kwenye machimbo yao na mawasiliano ya uhakika.

Naye Boniface Ishengoma mchimbaji mdogo wa madini alisema changamoto nyingine inayowafanya washindwe kuwekeza vizuri kwenye madini ya viwanda ni kwa wateja wao kutofuata bei elekezi ya serikali na hakuna watendaji wa serikali wanaofuatilia suala hilo pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika ya madini hayo.

Mwakilishi wa Kampuni ya Kioo, Joshua Zuberi, alisema kampuni yao ambayo ina inahitaji kwa kiasi kikubwa madini ya viwanda ili kuzalisha vifungashio vya chupa ambavyo vina soko katika nchi 17Afrika wakiwemo wateja wakubwa 100.

Zuberi alisema kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha vifungashio vya chupa milioni 320 kwa mwaka sawa na tani 145,000.

“Kampuni ya Kioo inatumia malighafi za ndani katika kutengeneza vifungashio vya chupa. Tunatumia mchanga, chokaa, magadi. Kwa mwaka tunatumia tani 70,000 za mchanga, tani 20,000 za chokaa na tani 24,000 za magadi. Kwa uzalishaji wa magadi Tanzania tuko nyuma, tunalazimika kuagiza magadi kutoka nchi jirani,”alisema Zuberi.

Dk Elisante Mshiu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alipendekeza Wizara ya Madini ipimwe kwa kiwango cha madini ya viwanda kinachozalishwa na siyo kiasi cha fedha inachoingiza.

Dk Mshiru alisema ikishajulikana kiwango cha madini ya viwanda kinachozalishwa, itaisaidia Wizara ya Viwanda nayo kujua viwanda vingapi vya madini ya viwanda vinahitajika nchini na hivyo kuvutia uwekezaji wa viwanda vya madini.

Januari 22, 2019 Rais Magufuli alikutana na wachimbaji wadogo wa madini jijini Dar es Salaam na kujadiliana nao kuhusu changamoto zao na suala la utoroshaji wa madini nje ya nchi.

Wachimbaji hao walimweleza Rais baadhi ya sababu zinazowafanya watoroshe madini kuwa ni pamoja na kuwepo kwa kodi na ushuru ambavyo hawakuwa na uwezo wa kuzilipa na ukosefu wa masoko ya uhakika.

Serikali ilizifanyia kazi changamoto hizo na kuziondoa kodi zote zilizokuwa kero kwao pamoja na kujenga masoko ya madini kwenye kila mkoa hali jambo lililosaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti utoroshaji wa madini.

Chanzo: habarileo.co.tz