0

‘Makaa ya mawe tani milioni 227 kuchimbwa kwa miaka 300 ijayo’

Sun, 18 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

MKOA wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 yanayotarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300, hatua ambayo imetajwa kuwa inathibitisha namna nchi ilivyo tajiri na inaweza kujiendesha kupitia sekta hiyo.

Sambamba na wingi wa madini hayo ambayo taarifa yake ilitolewa juzi na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Nkana, Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema nchi bado ina hazina kubwa ya madini mengine na serikali inajipanga kuyatumia kwa tija zaidi.

Waziri Biteko aliliambia gazeti hili juzi kwamba makaa mawe yameanza kuleta tija kubwa katika uchumi kwa kuwa ndiyo yanayotumika kuzalisha umeme katika viwanda vyote vya saruji na marumaru nchini.

Biteko alisema kwa miaka miwili sasa tangu kusitishwa uingizwaji wa makaa ya mawe nchini, kumekuwa na faida kubwa ya matumizi ya bidhaa hiyo ambayo imeshaanza pia kuuzwa kwa nchi jirani.

“Kwa sasa serikali inazidi kujipanga kutafuta uwekezaji mkubwa zaidi kwenye sekta ya makaa ya mawe ili kuhakikisha hicho kiasi kikubwa kinazidi kuinufaisha nchi kwa miaka mingi ijayo,” alisema Biteko.

Hazina makaa Kuhusu makaa ya mawe yaliyopo mkoani Ruvuma, Ofisa Madini Mkazi wa mkoa huo, Jumanne Nkana alisema utafiti na uchimbaji wake unafanyika katika wilaya mbalimbali.

Maeneo hayo na wilaya kwenye mabano ni Mbalawala na Mbuyula (Mbinga), Muhukuru, Njuga na Mtyangimbole (Songea) na maeneo ya Malini kata ya Mtipwili na Mbambabay wilayani Nyasa.

Nkana alisema utafiti wa awali wa makaa ya mawe ulifanyika katika maeneo ya Mbalawala na kubainika kuwa na tani milioni 99.5, Mbuyula walibaini tani milioni 15.1 na Muhukuru ni tani milioni 27.

Utafiti umebaini katika eneo la Njuga Wilaya ya Songea kuna tani milioni 23, Wilaya ya Nyasa maeneo ya Malini kata ya Mtipwili ni tani milioni 29. Kijiji cha Liweta Kata ya Mbaha walibaini tani milioni 34.

Kuhusu ubora wa makaa ya mawe yanayopatikana kwenye maeneo hayo, alisema yana wastani wa Calorific Value (CV) 5,000 hadi 7,000.

Hata hivyo alisema uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe unafanyika katika maeneo ya Mbalawala, Mbuyula, Mbambabay, Muhukulu na Liweta.

Alitaja wateja wakubwa wa makaa ya mawe yanayochimbwa katika maeneo hayo kwa sasa kuwa wapo ndani ya nchi na katika nchi jirani za Rwanda, Kenya na Uganda na kwamba wanatarajia kuanza kuuza makaa ya mawe India.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme aliagiza kampuni zinazochimba makaa ya mawe mkoani humo kuyauza kwenye viwanda vya ndani ili kupata nishati ya kutosha na ziada inayobaki isafirishwe kwenda nje ya nchi.

Mndeme ameagiza kampuni hizo pia zitoe ajira kwa Watanzania waweze kunufaika na rasilimali za nchi huku akisisitiza wachimbe makaa ya mawe yenye viwango soko lipanuke na wazingatie usalama na afya za watumishi wote wanaofanya kazi katika migodi husika.

Akizungumza na gazeti hili juu ya hazina ya makaa hayo ya mawe yaliyoko mkoani Ruvuma, mchambuzi na mchumi, Profesa Honest Ngowi alisema kuwa uwepo wa kiasi kikubwa cha madini hayo ni inshara kuwa nchi ni tajiri na inaweza kujiendesha kwa kiasi kikubwa kwa kutegemea madini.

Profesa Ngowi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, alishauri pawepo mkakati wa kuendeleza madini hayo kwa manufaa ya nchi. Vile vile ameshauri ufanyike uwekezaji mkubwa zaidi wa kundeleza madini hayo ya makaa ya mawe jambo ambalo Waziri Biteko amesema serikali imejipanga vyema.

Mikakati ya usimamizi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya uchaguzi ya mwaka 2020 - 2025, chama kinasema kitaelekeza Serikali kuendeleza rasilimali za asili za taifa ziweze kuchangia ipasavyo katika uchumi wa nchi na maendeleo ya watu wake.

Katika kueleza mafanikio ya miaka mitano chini ya ilani ya mwaka 2015- 2020, imeelezwa kwamba serikali ilisimamia mageuzi makubwa na ya kimkakati ikiwemo maboresho ya sheria na mifumo mbalimbali katika kuhakikisha sekta ya madini inaimarika kwa kiasi kikubwa na kuongeza mchango wake katika pato la taifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa ilani, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa makaa ya mawe na madini ya gesi kwa kuzuia uingizaji wa makaa ya mawe kutoka nje.

Hatua hiyo inatajwa kuwa imechangia kuongezeka uzalishaji wa madini hayo kwa ajili ya viwanda vya ndani vya saruji na watumiaji wengine.

Katika miaka mitano ijayo, CCM itaendelea kuisimamia serikali kuhakikisha mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya madini yanaendelezwa, hususan katika kuwewezesha wananchi kuwa sehemu ya umiliki wa rasilimali hiyo na kuhakikisha inachangia pato la taifa kupunguza umasikini nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz