0

Magwiji wa kilimo kuzungumzia mbolea kuleta mapinduzi ya kijani

Magwiji wa kilimo kuzungumzia mbolea kuleta mapinduzi ya kijani

Tue, 6 Oct 2020 Source: HabariLeo

J UMANNE ijayo Oktoba 13, eneo la Dakawa wilayani Mvomero, Morogoro, ambalo linasifi ka kitaifa kwa kilimo cha mpunga, litajiongezea sifa nyingine ya ziada ya kuwa kitovu cha sherehe ya Siku ya Mbolea Duniani.

Dakawa ni eneo lenye ardhi yenye rutuba lililowavuta wakulima wadogo zaidi ya 2,000 wanaojihusisha na kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji.

Siku hiyo eneo hilo lililoko kaskazini mwa mji wa Morogoro litawavuta wataalamu wabobezi katika kilimo kutoka serikalini, vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na utafiti, wafanyabiashara na wakulima wadogo.

Hawa watakaokusanyika kuadhimisha umuhimu wa mbolea katika kukuza kilimo na hivyo kutania wigo wa upatikanaji wa chakula ili kukidhi ongezeko la idadi ya watu.

Siku ya Mbolea Duniani huadhimishwa Oktoba 13 kila mwaka, ikiwa ni kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi aina ya amonia kinachopatikana hewani.

Uvumbuzi ambao ulifanywa mwaka 1908 na Bwana Fritz Haber na kupanda mbegu za Mapinduzi ya Kilimo mwanzoni wa karne ya 20. Lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kupata wigo mpana zaidi wa kuelezea masuala mbalimbali katika tasnia ya mbolea.

Masuala haya ni pamoja na mafanikio ya tasnia ya mbolea nchini mwetu, kuwaelimisha wadau wa mbolea, hususani wakulima na wafanyabiashara wa mbolea kuhusu mifumo mbalimbali ya upatikanaji na usambazaji wa mbolea.

Umuhimu wa mbolea Mbolea ni kirutubisho au mchanganyiko wa virutubisho (viinilishe) ambavyo huhitajika katika ukuaji na maendeleo ya mmea.

Mbolea hutumika ili kufidia upungufu wa virutubisho uliopo kwenye udongo. Mmea ukikosa virutubisho hivi hauwezi kukua na kutoa mavuno yenye tija.

Udhibiti wa mbolea Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuwezesha kilimo endelevu na chenye tija kwa wakulima kwa njia ya matumizi sahihi ya mbolea yenye ubora kwa ajili ya kuleta Mapinduzi ya Kijani.

Majukumu makubwa ya Mamlaka hii ni kudhibiti tasnia ya mbolea nchini, kudhibiti utengenezaji, uingizaji, usafirishaji na biashara ya mbolea, kusajili mbolea mpya, kusajili na kutoa leseni kwa wafanyabiashara wa mbolea, kutoa vibali vya utengenezaji, uingizaji, usambazaji wa mbolea nchini na nje ya nchi na kusimamia bei za mbolea.

Majukumu mengine ni kushirikiana na taasisi nyingine pamoja na mamlaka za serikali za mitaa katika kutoa ushauri wa kitaalamu na kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya mbolea.

Mamlaka pia ina jukumu la kuunganisha wauzaji na wanunuzi wa mbolea nchini ili kuhakikisha mbolea toshelevu inapatikana kwa wakati na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali na taasisi nyingine juu ya masuala yanayohusu sera za usimamizi na udhibiti wa ubora na biashara ya mbolea.

Tanzania imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu ambalo pia linasababisha kupungua maeneo ya mashamba. Ifikapo mwaka 2030, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu watakaofikia milioni 77.5.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephan Ngailo, anaonya kwamba idadi hiyo ya watu kwa miaka 10 ijayo itachagiza mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo ili kiweze kukidhi mahitaji ya chakula kutokana na ongezeko la watu.

“Mabadiliko hayo yatahitaji kilimo chenye tija kwa kutumia pembejeo bora za kilimo, ikiwemo mbolea, ili eneo dogo la kilimo liweze kutoa mazao mengi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula na malighafi katika viwanda,” anasema.

Dk Ngailo anasema upatikanaji wa pembejeo za kilimo, ikiwemo mbolea, utaimarisha na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo kama ilivyovyofafanuliwa kwenye Dira ya Maendeleo 2025.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018 kilimo kinaajiri asilimia 58 ya Watanzania. “Dira ya Maendeleo 2025 imepambanua mambo mengi ya kufikiwa ifikapo mwaka 2025.

Moja ya mambo hayo ni ujenzi wa uchumi wa viwanda. Zaidi ya asilimia 65 ya malighafi za viwandani zinatokana na kilimo.

Hivyo, kilimo chenye tija kwa matumizi bora ya mbolea kitahakikisha uwepo wa malighafi za kutosha katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini mwetu,” anaeleza Dk Ngailo.

Anasema serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali katika tasnia ya mbolea na kufanya sekta hii kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Mafanikio Mafanikio ya tasnia ya mbolea ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha ununuzi wa mbolea unaongezeka na wakulima wananufaika na punguzo la bei, kudhibiti mfumuko wa bei za mbolea, kusajili mbolea zote zinazotumika nchini, kuimarika kwa mifumo ya udhibiti na usambazaji wa mbolea, na kuondolewa kwa mbolea bandia.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa upatikanaji na matumizi ya mbolea na uzalishaji wa mazao, kuanzishwa kwa Mfumo wa Taarifa wa Kielektroniki, mfumo ambao utarahisisha upatikanaji wa huduma kwa mtandao.

“Hivyo wadau wetu wakiwemo wafanyabiashara wa mbolea, watengenezaji, waagizaji na wasafirishaji wa mbolea nje ya nchi hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu kupata huduma za vibali mbalimbali,” anaeleza Kaimu Meneja wa Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Nganga Nkoya.

Tanzania ambayo ni kitovu cha usambazaji wa mbolea katika mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa nchi ambazo hazina bandari, uzalishaji wa ndani wa mbolea ni asilimia 5 hadi 6 tu ya matumizi yote nchini.

Kwa mantiki hiyo, Nkoya anasema soko la mbolea ndani na nje ya Tanzania bado ni kubwa kwa sababu Tanzania imejaaliwa kuwa na malighafi za asili zinazoweza kutumika kwenye uzalishaji wa mbolea.

Moja ya malighafi hizo ni akiba ya tani milioni 8-10 ya madini ya fosifeti ya asili katika kijiji cha Minjingu, gesi asilia iliyopo Songo Songo mkoani Lindi na Mnazi Bay mkoani Mtwara. Isitoshe, serikali imebuni sera wezeshi katika tasnia ya mbolea ili kuwawezesha wadau katika tasnia hiyo, wakiwemo wafanyabiashara wa mbolea na wazalishaji wa mbolea.

Serikali pia imeondoa baadhi ya tozo na michakato ya kupata usajili kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara, hatua ambayo imechochea kupungua kwa bei ya mbolea.

Dk Ngailo anasema juhudi za Serikali katika uimarishaji wa tasnia ya mbolea kwa kushirikiana na sekta binafsi zimewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kwa wakulima ambako kumechochea ongezeko la tija na uzalishaji wa mazao.

“Hii imeongeza kipato cha mkulima, usalama wa chakula, kuongeza wigo wa upatikanaji wa malighafi za viwanda na kuongeza Pato la Taifa kutokana na uuzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi,” anasema Dk Ngailo.

Anaeleza kwamba matumizi sahihi ya mbolea katika sekta ya kilimo yataleta matokeo chanya katika sekta ya viwanda kwa kutoa mazao mengi ya biashara na chakula pamoja na malighafi za kutosha viwandani.

Anasema uwepo wa viwanda vya mbolea nchini utahamasisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei ya chini na hivyo kuongeza uzalishaji, tija na usalama wa chakula nchini, kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula na kuinua kipato cha mkulima.

Kwa mujibu wa Dk Ngailo, Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara yenye matumizi kidogo ya mbolea katika ngazi ya wakulima wadogo.

Anasema hali hiyo inachangiwa na sababu mbalimbali, hasa bei kubwa, upatikanaji wa mbolea na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa matumizi ya mbolea.

Kwa sasa matumizi ya mbolea ni kilo 19 za virutubisho kwa hekta, ambacho ni kiwango kidogo ikilinganishwa na kiwango kilichowekwa na Azimio la Maputo liliazimia kuongeza matumizi ya mbolea katika eneo la ukanda wa SADC kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2015.

Hali hii imeifanya Tanzania kufanya juhudi kubwa na kuweka mikakati mbalimbali kwa lengo la kutekeleza azimio hilo la Maputo ambalo imeliridhia kuongeza matumizi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji na tija.

Tangu mwaka 2016/17 hadi mwaka 2019/20, jumla ya mbolea zilizokuwa zimesajiliwa zilikuwa 103 na hivyo kuongeza kwa mbolea zilizohakikiwa kufaa kwake katika urutubishaji wa mimea.

Sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wakaguzi na usajili wa mbolea, jumla ya wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni walikuwa kati ya 632 mwaka 2016/7 lakini wameongezeka hadi kufikia 1,501 mwaka 2018/2019.

“Hadi sasa mbolea zisizokidhi viwango au bandia zimepungua kwa kiasi kikubwa katika masoko.

Kazi hii ya kudhibiti imekuwa ikifanyika kwa kuimarisha ukaguzi, kutambua wafanyabiashara wote kwa kuwasajili, kuwafuatilia na kutoa elimu juu ya utunzaji bora wa mbolea na jinsi gani ya kutambua mbolea zisizokidhi viwango,” anaeleza Dk Ngailo.

Anasema matumizi ya mbolea yameongezeka na hivyo kuongeza uzalishaji. Mwaka 2015/16 matumizi ya mbolea yalikuwa tani 296,036 na mwaka 2018/9 matumizi ya mbolea yalikuwa tani 364,968.

Ongezeko hili ni sawa na asilimia 23 na “limetokana na serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuanzisha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja ulioanza kutumika msimu wa kilimo 2017/2018 na kuwawezesha wakulima wadogo kutumia mbolea zaidi kutokana na kupata punguzo la bei za mbolea litokanalo na kununua na kusafirisha baharini mbolea nyingi kwa wakati Mmoja,” anaeleza Nkoya.

Chanzo: HabariLeo