0

Magufuli afuta ushuru Soko la Ndizi

Tue, 13 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli amefuta ushuru katika soko la Urafiki maarufu ‘Mahakama ya ndizi’ na badala yake amewataka wafanyabiashara kwenye soko hilo kununua vitambulisho vya machinga ambavyo vinapatikana kwa Shilingi 20,000.

Magufuli ameyasema hayo leo uwanja wa Barafu Mburahati, katika kampeni zake za kuwania ngwe ya pili ya urais.

Pia mbali na kuwataka kutolipa ushuru, vilevile amekabidhi soko hilo kuanzia sasa kuwa chini ya wananchi.

“Kwa mamlaka niliyonayo kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninafuta ushuru wa soko la Mahakama ya ndizi, na kama kuna taratibu nyingine za sheria ya ardhi namba nne na tano ya mwaka 1996, na ile ya matumizi bora ya ardhi ya mwaka 2007, yafanyike mara moja ili soko ilo libaki chini ya umiliki wa wananchi,” amesema

Awali eneo hilo la soko lilikuwa likimilikiwa na Kiwanda cha Urafiki.

“Natamka wanaofanya biashara pale asitokee mtu yoyote kuwabugudhi wafanyabiashara wa soko hilo, ambao watakuwa na vitambulisho”.

Katika hatua nyingine Magufuli amewataka wananchi wa Mburahati kuwachagua wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM, katika Wilaya ya Ubungo ili waweze kujengewa majengo ya makao makuu ya Wilaya hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz