0

Machinga, mamalishe, bodaboda wafurahia ushindi wa Magufuli

Machinga, mamalishe, bodaboda wafurahia ushindi wa Magufuli

Sun, 1 Nov 2020 Source: HabariLeo

Wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo wamachinga, bodaboda, mama lishe na makundi ya vijana wamempongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi.

Wamesema ushindi huo mkubwa, unaonesha kuwa Watanzania wanamuamini, kutokana na yale aliyoyafanya katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano na ahadi alizotoa za kuwaletea wananchi maendeleo zaidi .

Wameeleza kuwa wanafurahia ushindi huo na wana matarajio makubwa na uongozi wa Rais Magufuli kwa miaka mitano tena.

Walisema hayo kwa nyakati tofauti jana mjini Morogoro, walipokuwa wakitoa maoni yao kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Walisema baada ya mshindi halali wa uchaguzi wa rais kutangazwa, sasa wanaelekeza nguvu zao katika shughuli za maendeleo.

Walisisitiza kuwa hawako tayari kutumiwa na baadhi ya wanasiasa, ambao wanahamasisha vijana washiriki kufanya maandamano na pia hawako tayari kurudishwa nyuma kimaendeleo, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Walieleza kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu mkubwa na mshindi wa kiti cha urais kupatikana, ambaye ni Dk Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Athuman Salum maarufu kwa jina la Chinga alieleza kuwa uchaguzi wa mwaka huu, ulikuwa huru na haki kutokana na uwazi uliokuwepo siku ya upigaji kura. Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitoa elimu ya kutosha, hivyo kurahisha wapigakura kuchagua wagombea wanaowataka .

Alisema pia wananchi akiwemo yeye walisikiliza vizuri sera za wagombea, ambazo ndizo zimewawezesha kufanya maamuzi. Hivyo, alisema waliochaguliwa wamepita kihalali.

Mama lishe, Nuru Hatibu alisema suala la kuandamana litawaletea madhara makubwa watakaoandamana na familia zao. Alitaka watu kuendelea na shughuli zao za kila siku na kujiingizia kipato chao .

Mkazi mwingine wa Mtaa wa Amani Kata ya Mji Mkuu mjini Morogoro, Idrisa Juma, alisema uchaguzi umemalizika salama na kuwataka Watanzania waendelee kuijenga nchi.

Mkazi wa Kata ya Kilakala, Wilchester Matu na wenzake Dotto Evarist, Kulwa John, Alphone Zacharia, Juma Ndeka, Mohamed Hamis na Iddi Juma nao kwa nyakati tofauti walimshukuru Mungu kwa kuwezesha uchaguzi kumalizika kwa amani. Walisema baada ya uchaguzi, kuna kazi za kufanya kama za kuuza nguo na biashara nyingine.

Chanzo: HabariLeo