0

Kiwanda cha ngozi kujengwa kwa bil 3.3/-

Thu, 15 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

KIWANDA cha kuchakata ngozi kinatarajiwa kujengwa katika halmashauri ya Bahi mkoani Dodoma ambapo ujenzi wake utagharimu Sh bilioni 3.3.

Wilaya hiyo ina jumla ya ng'ombe 294,235, mbuzi 156,365, kondoo 61,112, Punda 9,443, nguruwe 3,504, kuku 327,300, bata 2,912 na kanga 2,623.

Hayo yalibainika juzi wakati wa uzinduzi wa uogeshaji mifugo awamu ya tatu kwa lengo kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe uliofanyika kijiji cha Bahi Sokoni.

Mkuu wa Idara ya mifugo na uvuvi katika halmashauri ya Bahi, Daniel Kehogo akitoa taarifa mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante ole Gabriel alisema sekta ya ngozi ni miongoni mwa fursa kubwa za uwekezaji katika wilaya hiyo kutokana na wingi wa mifugo inayochinjwa kwa mwaka.

Alisema wastani wa ng'ombe 1,085, mbuzi na kondoo 2,245 huchinjwa kwa mwezi hivyo kuna fursa kubwa ya uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa vya kusindika na kuchakata ngozi na mazao yake.

"Halmashauri imekwishaandika andiko la mradi wa kiwanda cha kuchakata ngozi lenye thamani ya Sh bilioni 3.3, tayari andiko hilo liko Wizara ya Fedha kwa ajili ya mapitio ya mwisho kabla ya fedha kutolewa," alisema.

Pia alisema wilaya hiyo ina miundombinu mbalimbali ya mifugo yakiwemo majosho, malambo, machinjio, mabucha, mabwawa ya samaki na minada.

Alisema baadhi ya miundombinu kama malambo na majosho ni ya muda mrefu hivyo yanahitaji ukarabati ili yaendelee kufanya kazi, halmashauri inaendelea kukarabati na kujenga miundombinu mipya kadri ya upatikanaji wa fedha na makusanyo ya ndani, washirika wa maendeleo na za miradi ya maendeleo kutoka serikali kuu.

Alisema katika wilaya hiyo eneo linalofaa kwa ajili ya malisho ni hekta 133,156 kulinganisha na uwiano wa kitaifa ambao ni mnyama moja kwa hekta 2 hadi tatu kwa mwaka.

"Eneo hili linatosheleza kwa ng'ombe 44,385 na hivyo kufanya zidio la ng'ombe 249,850, eneo lililopo halitoshi kutokana na mifugo iliyopo hivyo kuwahamasisha wafugaji kuvuna mifugo yao ili kupunguza idadi ya mifugo iendane na eneo lilipo kwa ajili ya ufugaji," alisema.

Aidha alisema magonjwa ya mifugo ni miongoni mwa changamoto inayowakabili wafugaji na magonjwa yanayosumbua ni yale yanayoenezwa na kupe kama ndigana kali, ndigana baridi, ugonjwa wa mapafu kwa ng'ombe na mbuzi, kideri kwa kuku.

Alisema udhibiti wa magonjwa ya mifugo hufanyika kwa kuogesha na kunyunyizia mifugo viuatilifu, kutoa chanjo, kutoa ushauri wa kitaalamu kupitia maofisa ugani waliopo katika kata na vijiji.

Katibu Tawala Wilaya ya Bahi, Jeremia Mapogo alisema wana fursa kubwa ya kulisha Jiji la Dodoma kupitia mifugo.

Alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wafugaji juu ya uvunaji mifugo sambamba na kuendelea kwa ujenzi wa mabwawa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wizara ya Mifugo Profesa Elisante ole Gabriel aliunga mkono juhudi za halmashauri hiyo kuwa na kiwanda cha kuchakata ngozi kwani ni moja ya uwekezaji kwenye sekta ya mifugo.

Chanzo: habarileo.co.tz