0

Hizi ndizo sababu za kupanda bei ya saruji Pwani

87830f85a8e367e8fb87184d7cec75e2 Hizi ndizo sababu za kupanda bei ya saruji Pwani

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

Upungufu wa saruji uliojitokeza hapa nchini kutokana na baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati haujaathiri ujenzi wa miradi mikubwa ya ya Kitaifa ya kimkakati kwenye mkoa wa Pwani.

Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo akiwa na uongozi wa wilaya ya Kibaha walipofanya ziara kutembelea wauzaji wakubwa wa saruji kwenye mji wa Kibaha.

Ndikilo alisema kuwa kwa muda sasa kumekuwa na upungufu mkubwa wa saruji kwenye mkoa huo lakini hata hivyo upungufu huo haujaathiri ujenzi wa miradi hiyo mikubwa hapa nchini.

“Nimetembelea na kujionea mwenyewe changamoto ya upungufu wa saruji lakini hakuna athari ambazo zimejitokeza kwenye ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na ule wa uzalishaji umeme kule Rufiji wa Nyerere, ujenzi wa reli ya mwendokasi ya (SGR) na ujenzi wa barababara kutoka Jijini Dar es Salaam kuja Kibaha lakini wajenzi wanaendelea na kazi zao,”alisema Ndikilo.

Alisema kuwa mahitaji mkoa wa Pwani mahitaji makubwa sana kutokana na miradi mikubwa pamoja na ujenzi wa viwanda ambavyo vinajengwa kwa kasi kubwa.

Moja ya wauzaji waliozunguza na waandishi wa habari Denis Magese ambaye ni ofisa masoko kutoka kampuni ya VGK kanda ya Kibaha alisema kuwa kwa sasa saruji ni upungufu mkubwa ambapo kwa sasa wanadaiwa tani 300 kwa wateja ambao tayari walishalipia lakini kutokana na uhaba huo wanasubiri.

Naye muuzaji wa saruji Rahel Msaki alisema kuwa kwa sasa wanakaribia mwezi mzima hawana saruji na wanapowauliza mawakala wanaowaletea wanasema kuwa huko viwandani wanaambiwa kuna foleni kubwa hivyo wasubiri na hawajui wasubiri kwa muda gani.

Kwa upande wake Halfan Mwanga alisema kuwa hawaelewi tatizo kubwa lililopo ambapo wengine wanasema kuna baadhi ya malighafi hazipo mara wengine wanasema ni ukarabati hivyo kuna haja ya serikali kukaa na wenye viwanda ili wajue tatizo liko wapi lakini kwa upande wao hawana tatizo na bei wanayouza ni ile iliyopangwa na serikali.

Chanzo: HabariLeo