0

Ewura na Latra wasaini mkataba wa ushirikiano

Ewura na Latra wasaini mkataba wa ushirikiano

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Mafuta na Maji nchini (EWURA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA) wamesaini mkataba wa makubaliano wa kushirikiana ili kila mmoja atimize majukumu yake na kufahamu mipaka baina yao.

Kadhalika, kuanza kwa mkataba huo kunafungua ukurasa rasmi wa udhibiti wa madereva wanaoendesha magari ya mafuta ambao watatakiwa kuwa na mafunzo maalumu ya uendeshaji na kisha kuhakikiwa kabla ya kupewe idhini ya kuendesha vyombo hivyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kwenye hafla ya utiaji saini mkataba huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ewura, Ahmed Kilima alisema mkataba huo utaonesha mipaka ya mamlaka hizo kiutendaji kuepuka kuingilia majukumu ya mwingine.

Kilima alisema mkataba huo ni chachu ya kudhibiti ubora wa huduma na bidhaa na kwamba umekuja wakati nzuri ili pia kudhibiti matukio ya ajali za magari ya mafuta zinazogharimu maisha na mali za wananchi.

Akizungumzia manufaa ya mkataba huo, Kilima alisema itaondoa maeneo waliyokuwa wakiingiliana kiutendaji kati yao na LATRA, hivyo kila pande itatimiza wajibu wake kwa viwango.

Kuhusu udhibiti wa madereva wa magari ya mafuta, Kilima alisema wanazungumza na wadau wengine ambao ni Polisi na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kuwafundisha madevera kozi maalumu ya kuboresha fani yao na kuwa na ujuzi na sifa za kuendesha magari hayo.

"Tutazungumza na Polisi wa Usalama Barabarani wawe na tahadhari, wanaposimamisha magari ya mafuta wajue wamesimamisha bomu linaloweza kulipuka wakati wowote na kuleta madhara kwa watu na mali,"alisema Kilima.

Akizungumzia udhibiti wa magari ya mafuta, Mkurugenzi wa LATRA, Gilliard Ngewe alisema kufikiwa kwa mkataba huo ni ufunguo muhimu wa kuhakikisha majukumu ya pande mbili hizo yanatekelezwa bila mkwamo.

Chanzo: HabariLeo