0

DCB yawagawia milioni 287 wanahisa watatu

Fri, 23 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

BENKI ya Biashara ya DCB imetoa gawio la Sh milioni 287 kwa wana hisa wake wakubwa watatu.

Katika gawio hilo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejinyakulia Sh milioni 138 huku Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja (UTT-Asset Management and Investor Services - UTT-Amis) ukipata gawio la Sh milioni 119. Sh milioni 30.8 zimelipwa kama gawio kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Fedha hizo ni sehemu ya gawio la jumla la Sh milioni 500 ambazo benki ya DCB itawalipa wawekezaji wake kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 18 wa wanahisa uliofanyika kwa njia ya mtandao Juni mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa, alisema: “Ikiwa ni miaka mitatu tangu kuanza safari hii, tumefanikiwa kurudi kwenye faida mwaka 2018 na tumekuwa tukijiendesha kwa faida hadi sasa.

Vilevile, benki imefanikiwa kuongeza mtaji kupitia uuzwaji wa hisa mwaka 2019 na kuendelea kujiimarisha zaidi… Akaongeza: “Benki yetu ipo imara kimtaji, kupungua mikopo chechefu, kuongezeka kwa ukwasi na uendeshaji bora huku ikifuata taratibu na miongozo ya usimamizi wa Benki Kuu na mamlaka nyingine za usimamizi za serikali.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo aliipongeza menejimenti ya DCB kufanikisha utoaji wa gawio kwa wanahisa wake wakuu.

“Naipongeza DCB kwa mafanikio makubwa iliyopata kwa miaka 14 tangu kuanzishwa kwake. Natambua kuwa benki hii imeanzishwa kwa malengo ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wananchi wa kawaida ili wajikwamue kutoka kwenye umasikini,” alisema.

Kwa mujibu wa Jafo, benki hiyo ilijiendesha kwa faida kwa miaka takribani 12 huku ikitoa gawio kwa wanahisa kwa miaka 10 mfululizo, kiasi kinachofikia Sh bilioni 12.

Chanzo: habarileo.co.tz