0

Bei ya saruji yashuka Dar

Bei ya saruji yashuka Dar

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amesema bei ya rejareja saruji imeanza kushuka na baadhi ya wauzaji waliokuwa wakilangua wanahojiwa Polisi.

Ameviagiza vyombo vya ulinzi kuendelea kuwakamata walanguzi wanaoendelea kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu.

Juzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza wakuu wote wa mikoa wafuatilie kubaini sababu za kupanda bei ya saruji wawe wamempa taarifa ifikapo keshokutwa Ijumaa.

Alitoa agizo hilo katika viwanja vya Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma baada ya Rais John Magufuli kumuapisha kuendelea na wadhifa huo.

Kunenge alisema hakuna sababu ya bei kuendelea kuwa juu wakati kiwandani bei haijapanda.

“Serikali ya mkoa kamwe haiwezi kuwanyamazia watu hawa, ni lazima washughulikiwe kwa kila namna kwa kuwa huu ni wizi wanaoufanya kwa wananchi, ninasisitiza kwa wale wanaoendelea kuwaibia wananchi serikali itawashughulikia ipasavyo. Nimeambiwa kuwa wapo ambao walikamatwa kwa kulangua saruji na ninataka walanguzi kuacha mara moja kabla hawajachukuliwa hatua zaidi,” alisema Kunenge.

Ufuatiliaji uliofanywa na gazeti hili Wilaya ya Temeke katika maeneo ya Tandika maduka yanayouza saruji bei ilikuwa ni Sh 16,000 kwa mfuko, na kwa mujibu wa wauzaji ni bei iliyoanza tangu wiki iliyopita.

Meneja Mauzo Mwandamizi wa Kampuni ya Twiga Cement, Danford Semwenda alisema kampuni hiyo imepunguza kiwango cha saruji kwenda nchi jirani ya Rwanda kutoka tani 40,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 20,000.

Alisema kiwanda hicho kinaweza kuzalisha hadi tani 6,000 kwa siku hivyo kwa mwezi kinazalisha hadi tani 60,000.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema atatoa majibu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu atakapofanya uchunguzi na kupata majibu.

Akizungumza kwa simu jana, Byakanwa alisema kwa sasa yupo Dodoma na kwamba hawezi kutoa majibu sahihi kuhusiana na agizo hilo la Waziri Mkuu.

Hivi karibuni, Byakanwa alitembelea kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote mkoani Mtwara na akawataka na kuwataka wasimamizi wa kiwanda hicho watangaze bei ya bidhaa hiyo.

“Nimewataka watangaze kwenye magazeti ili wananchi wote wajua kwamba bei yetu ya 'cement' inapaswa kuwa hii na akikuta imepanda asinunue atoe taarifa kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya na pengine wakuu wa mikoa tuwatafute hao wafanyabiashara ambao wanataka kupata faida kinyume na utaratibu,” alisema Byakanwa.

. Imeandikwa na Anne Robi (Mtwara), Evance Ng’ingo (Dar es Salaam)

Chanzo: HabariLeo