0

Bandari ya Dar yatwaa tuzo ubora Afrika 2020

Bandari ya Dar yatwaa tuzo ubora Afrika 2020

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

BANDARI ya Dar es Salaam imetwaa tuzo ya dunia kwa kuwa Bandari Bora Afrika kwa safari za mapumziko na kuburudika mwaka 2020.

Katika tuzo hizo za kila mwaka zinazotolewa na Taasisi ya Word Travel Awards (WTA) ya Marekani, bandari hiyo imezishinda bandari za Elizabeth, Cape Town, Durban za Afrika Kusini, Bandari ya Mombasa, Kenya na Bandari ya Zanzibar.

Katika miaka mitano iliyopita Bandari ya Durban ilishinda tuzo hiyo mara mbili (2018, 2019), na Bandari ya Mombasa ilishinda mara tatu (2015, 2016, 2017).

Uongozi Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) jana uliipongeza bandari hiyo kwa kupata tuzo.

“Ni ushindi mkubwa kwa Tanzania na Bodi ya Utalii kwani unapanua wigo wa mazao ya utalii ambapo Cruise Ship Tourism ni zao linalopendwa duniani,” alisema mmoja wa viongozi wa TTB ambaye hakutaka kutajwa gazetini

Tuzo ya Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwa tuzo sita ilizopata Tanzania kwenye tuzo hizo za dunia mwaka huu ikiwemo ile ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo imekuwa hifadhi bora Afrika mwaka 2020.

Taarifa ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), anayeshughulika na Mawasiliano, Pascal Shelutete, ilieleza kuwa ni mara ya pili kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushinda katika kundi la hifadhi zinazoongoza kwa ubora Afrika.

Shelutete alieleza kuwa hifadhi hiyo ilizishinda hifadhi tano za Afrika ikiwemo Hifadhi ya Central Kalahari-Botswana, Etosha-Namibia , Kidepo Valley-Uganda, Kluger-Afrika Kusini na Masai Mara -Kenya.

Alisema hifadhi hiyo inajivunia umaarufu wa msafara wa nyumbu zaidi ya milioni 1.5 wanaohama, aina za wanyamapori wanaopatikana kwa wingi, mandhari nzuri ya kuvutia na shughuli za utalii zinazovutia watalii wengi.

Tuzo zinazotolewa na WTA zilianza kutolewa mwaka 1993 ili kuwatambua, kuwatuza waliofanya vizuri kwenye sekta zote zinazohusiana na safari, utalii na huduma.

Washindi kwenye mabara watashindanishwa kwenye vipengele vinavyofanana kidunia na washindi watatangazwa kwenye hafla ya fainali ya tuzo hizo jijini Moscow nchini Russia.

Chanzo: HabariLeo