0

Ashauri usimamizi imara vyama vya saccos

Wed, 21 Oct 2020 Source: habarileo.co.tz

WITO umetolewa kwa maofisa Ushirika Manispaa ya Ilala, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Manispaa ya Ilala na COASCO kufanya ufuatiliaji, ukaguzi na usimamizi wa karibu ili kuhakikisha sheria na taratibu za saccos na vikoba zinafuatwa.

Wito huo ulitolewa na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Christopher Myava mbele ya waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam juzi.

Alisema Takukuru imedhibiti upotevu wa fedha milioni 35.6 kutoka kwa wadaiwa sugu wa Vikoba na Saccos na kuzirudisha kwa wahusika.

Alisema Takukuru Mkoa wa Ilala ilifanikiwa kuokoa kiasi hicho baada ya kupokea taarifa mbalimbali na kuzifanyia uchunguzi kuhusiana na vikoba na saccos.

“Takukuru Mkoa wa Ilala imekuwa ikipokea taarifa na kufanya uchunguzi mbalimbali kuhusu saccos na Vikoba ambapo imeonekana kuwa saccos nyingi zina tatizo la wanachama kuchukua mikopo mikubwa ambayo wanashindwa kuirejesha kwa wakati, kukosekana kwa fedha pale wanachama wanapostaafu ama kujitoa, matumizi makubwa ya watendaji waliopo kwenye saccos na kutokufuatwa kwa sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza vyama vya ushirika zikiwemo saccos na vikoba,” alisema Myava.

Alisema katika kuhakikisha kero mbalimbali zinapatiwa ufumbuzi na kupata njia sahihi ya kuishauri serikali kuhusiana na masuala ya rushwa, wamefanya uchambuzi wa mfumo wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kubaini kuwa wakopaji wanahusiana na wanasiasa na watumishi wa Manispaa hali iliyosababisha mikopo kutorejeshwa.

Alisema kutokuwa makini kwa wasimamizi katika kuhakiki wakopaji na kusimamia marejesho kumesababisha zaidi ya Sh bilioni 2.6 kutorejeshwa kwa wakati.

Myava alisema ofisi yake imefuatilia matumizi ya fesha za umma kwenye miradi ya maji Kisarawe- Gongolamboto wenye thamani ya Sh bilioni 7.3 na mradi wa kukamilisha ujenzi wa jingo la ofisi za mtaa wa Mzinga wenye thamani ya Sh milioni 35. Alisema ufuatiliaji huo umekamalika na yametolewa mapendekezo kwa ajili ya uchunguzi.

“Pamoja na kuchambua mfumo pia ofisi imefuatilia matumizi ya fedha za umma (PETS) kwenye miradi wa maji wa Kisarawe–Gongolamboto wenye thamani ya Sh 7,370,378,901.45 na kuongeza ufanisi na kasi ya ufuatiliaji mradi; ufuatiliaji mradi wa kukamilisha ujenzi wa jengo la ofisi za mtaa wa Mzinga wenye thamani ya milioni 35 ambapo ufuatialiji huu umekamika na mapendekezo yametolewa kwa ajili ya hatua za uchuguzi,” alisema Myava.

Chanzo: habarileo.co.tz