0

Utata mazishi ya Aurlus Mabele

Thu, 26 Mar 2020 Source: mwananchi.co.tz

Brazaville, Kongo. Siku mbili baada ya kifo cha mwanamuziki maarufu wa Jamhuri ya Kongo, Aurulus Mabele, mazungumzo kati ya familia yake na serikali yameanza ili kuruhusu azikwe nyumbani, lakini kipingamizi kwa sasa ni ugonjwa wa corona.

Mabele alifariki dunia juzi jijini Paris, Ufaransa kwa kilichoelezwa kuwa ni kutokana na ugonjwa wa corona. Pia mwanamuziki huyo wa miondoko ya soukous alikuwa akisumbuliwa na kansa ya koo kwa zaidi ya miaka 10.

Kwa sasa mwili wake hauwezi kurejeshwa Brazaville, Kongo, alikozaliwa mpaka zuio la usafiri kutoka nje ya nchi hiyo litakapoondolewa na serikali ama familia yake ipate kibali maalumu cha kuusafirisha chini ya usimamizi wa mamlaka za serikali.

Habari kutoka Brazaville zilisema jana kuwa, kuna zuio la usafiri wa ndege kutoka nje ya nchi lililotangazwa siku 10 zilizopita kutokana na tishio la corona, ambapo hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia kutoka nje ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa zuio hilo, watu wanaotaka kuingia Kongo wanatakiwa kuomba kibali maalumu serikalini kinachoidhinishwa na Waziri wa Afya au Usalama baada ya majadiliano na kwamba, mara baada ya kuruhusiwa wahusika wanapaswa kujiweka karantini kwa wiki mbili kabla ya kuruhusiwa kuchangamana na raia.

Kutokana na hali hiyo, urejeshaji wa mwili wa mwanamuziki huyo huenda ukakumbana na ugumu ikizingatiwa kuwa mbali ya kwamba alikuwa mgonjwa muda mrefu akisumbuliwa na magonjwa mengine, corona ndio ugonjwa unaotajwa kumuua na ndio ulioifanya Kongo kupiga marufuku wageni kuingia nchini humo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Taarifa za kifo cha mwanamuziki huyo zilitangazwa juzi na bintiye Liza Monet ambaye pia ni mwanamuziki, aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter na Facebook akisema baba yake amefariki kutokana na corona sawa na alivyofanya mpwawe, Robert Mabele aliyesema mjomba wake amefariki.

Kabla ya kukumbwa na mauti, mbali na kansa ya koo pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya muda mrefu yaliyomuweka kitandani kwa miaka mingi sambamba na kupooza, ambapo hali ya udhaifu wa mwili ilisababisha ashindwe kukabiliana na corona baada ya ugonjwa huo kumpata siku chache zilizopita.

Mashabiki wa muziki wa Kongo walimfahamu kupitia Kundi la Loketo lililojumuisha magwiji na nyota mbalimbali wa muziki barani Afrika hasa kutoka nchi za DR Congo na Kongo -Brazzaville. Baadhi ya albamu zilizomtangaza ni Soukous la Terreur (1991), Stop Arretez (1993), Tour de Controle (1999), Dossier X (2000) na Fiesta d’Or aliyoifyatua 2002.

Chanzo: mwananchi.co.tz