0
MenuDunia
Afrika

Simba yaja na vita kamili kwa Al Ahly

Simba yaja na vita kamili kwa Al Ahly

Sat, 20 Feb 2021 Source: HabariLeo

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wametangaza ‘vita kamili’ kwa wapinzani wao Al Ahly ya Misri wakisema wanao uwezo wa kuwafunga Jumanne.

Simba itakutana na mabingwa hao watetezi wa Afrika katika mchezo wa pili wa kundi A la michuano hiyo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana msemaji wa Simba Haji Manara alisema wanajua kuwa Al Ahly ni timu kubwa na sio kiwango chao lakini wao wamejipanga kushinda mchezo huo ndani na nje ya uwanja hivyo ni lazima watimize lengo.

“Mara ya mwisho tulikutana hapa Dar tukawafunga bao 1-0 kwenye mechi tuliyosema Yes we can na tukaweza. Al Ahly mara zote tukicheza Tanzania tunawafunga, Dhamira hiyo ipo kwa kila Mwanasimba kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama na mashabiki wote.”alisema.

Manara alisema mechi ya mwisho kwenye uwanja wa nyumbani waliita Vita Dar es Salaam sasa wanakuja na nyingine ‘Vita kamili, hakuna kurudi nyuma’ akisema wapinzani wao ni mabingwa wa Afrika, wanajua ukubwa wao ila Simba ina malengo yake ni muhimu ipate pointi tatu.

“Tunataka kuleta heshima kwa Afrika Mashariki. Tunawakilisha zaidi ya watu milioni 150 na wote hao wanategemea timu moja Simba, tunaenda kutetea timu, Tanzania na Afrika Mashariki yote.”alisema.

Alisema kama waliweza kuifunga AS Vita kwao bao 1-0 ambao msimu wa mwaka juzi iliwachapa mabao 5-0, hata Al Ahly wataweza huku akitolea mfano kuwa Simba iliwahi kuzifunga timu mbalimbali kubwa nyumbani kama Zamalek, Ismailia, Arab Contractor miaka ya zamani.

Msemaji huyo alitaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh. 3000 kwa viti vya mzunguko, Sh 15,000 VIP B na Sh 30,000 kwa VIP A na kwamba tiketi zimeshaanza kuuzwa tangu jana na zitaendelea hadi keshokutwa.

Alisema mashabiki wanaohitajika uwanjani kwa mujibu wa utaratibu wa Shirikisho la soka Afrika (Caf) ni 30,000 hivyo wale watakaochelewa kununua tiketi mapema hadi siku ya mchezo viwango vitaongezeka Sh. 5000 kwa viti vya mzunguko, Sh 20,000 kwa VIP B na Sh 40,000 kwa VIP A.

Mkuu wa Kitengo cha masoko wa klabu hiyo George Abdulrahman alisema “tumesikia changamoto ya vituo vya kuuza tiketi na sasa tumejipanga vizuri, tunawafikia kila sehemu na Jumamosi (leo) tutakuwa tunawafuata mtaani.”

Aliwataka mashabiki watakaoingia uwanjani kuchukua tahadhari za Covid-19 kwa kuhakikisha wanapeana nafasi ya kiti kimoja.

Chanzo: HabariLeo