0
MenuDunia
Afrika

Shambulizi shuleni laua mmoja, 27 watekwa

Shambulizi shuleni laua mmoja, 27 watekwa

Fri, 19 Feb 2021 Source: HabariLeo

WATU wenye silaha wamevamia shule ya wavulana ya bweni na kuwashambulia kwa risasi zilizosababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na kuwateka wengine 27 katika eneo la Kagara, Kaskazini-kati mwa Nigeria.

Gavana wa eneo hilo, Abubakar Bello alithibitisha shambulio hilo na kueleza kuwa, wafanyakazi watatu na ndugu zao 12 pia walitekwa nyara katika shambulio hilo lililotekelezwa usiku.

Mkuu wa Shule, Danasabe Ubaidu, alisema takribani wanafunzi 600 walikuwa wamelala katika mabweni yao wakati shule hiyo iliyopo katika mji wa Kagara, Jimbo la Niger, ilipovamiwa.

Vikosi vya usalama vilipelekwa eneo la tukio kusaidia shughuli za uokoaji.

Hata hivyo sababu za shambulio hilo na utekaji hazijajulikana.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, amevitaka vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo kufanya juhudi zote kuwanusuru waliotekwa.

Jumatatu, watu 20 waliokuwa wakitoka katika sherehe za harusi walitekwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kushambuliwa katika Jimbo la Niger.

Desemba mwaka jana, wanafunzi wavulana zaidi ya 300 walitekwa katika mji wa Kankara eneo la Kaskazini-Magharibi mwa Jimbo la Katsina. Baadaye, waliachiwa huru baada ya mazungumzo na watekaji.

Katika shambulio la hivi karibuni, watekaji nyara walikuwa wamevaa sare za jeshi na kuvamia shule ya kulala ya wavulana wengi inayoendeshwa na serikali ya jimbo, kabla ya kuwachukua wanafunzi hao katika msitu uliopo karibu.

Chanzo: HabariLeo