0

Rwanda yaanza kutoa chanjo ya covid-19

Rwanda yaanza kutoa chanjo ya covid-19

Tue, 23 Feb 2021 Source: HabariLeo

SERIKALI imeanza mpango wa kitaifa wa kutoa chanjo ya covid-19 kwa kuanza na wafanyakazi wa huduma ya afya kama sehemu ya makundi yaliyo hatarini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, chanjo hizo zimeidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO) zimepatikana kupitia ushirikiano wa kimataifa.

"Rwanda iko tayari kwa chanjo ya covid-19, tayari imewekwa miundombinu, itifaki na wafanyakazi wapo," ilisema taarifa hiyo na kueleza kuwa mpango wa kitaifa wa chanjo unatarajiwa kufanywa kwa awamu.

Ilisema awamu ya kwanza, chanjo hiyo itatolewa kwa wafanyakazi walio mstari wa mbele katika huduma za afya wakiwemo wanaofanya kazi katika vituo vya matibabu na vitengo vya uangaliazi maalum (ICUs).

“Awamu hii pia chanjo itatolewa kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 65 na wale ambao kinga yao ni dhaifu na ina kunauwezekano wa kuathirika kwa urahisi kama wenye magonjwa ya saratani, kisukari, ukimwi magonjwa mengine,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema makundi mengine yanayopaswa kuzingatiwa ni kwa sababu ya udhaifu wao ni kama wafungwa magerezani, wakimbizi na wafanyakazi wa usalama ambao wanakabiliwa na hatari ya kuambuklizwa virusi kwa njia moja au nyingine.

Rwanda, DRC zakubaliana kushughulikia waasi-LEAD

KIGALI

RWANDA na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika masuala ya usalama na kushungulikia waasi wanaofanya ghasia katika maeneo ya Mashariki.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkutano wa siku mbili wa maofisa wa usalama kutoka nchi hizo mbili uliofanyika katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Katika mazungumzo hayo, maofisa waandamizi wa usalama kutoka DRC waliongozwa na mshauri maalum wa masuala ya usalama wa Rais, Francois Beya, huku Rwanda, wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi, Jenerali Bosco Kazura na kubuni mfumo wa kushughulikia vitisho vya usalama vinavyoathiri nchi zote mbili.

Maofisa hao wametoka na mapendekezo kadhaa na mpango wa utekelezaji wa haraka unaolenga kurejesha amani Mashariki mwa DRC.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda ilieleza kuwa, mkutano huo uliitishwa kufuatia ghasia mpya za watu wanaodaiwa kuwa waasi wa Uganda wa kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF) Mashariki mwa DRC.

Wiki iliyopita waasi waliwaua watu 10 na kuwateka nyara wengine kadhaa katika uvamizi wa kijiji cha Mabule karibu kilomita 25 (maili 16) Kusini Mashariki mwa mji wa Beni nchini DRC.

Akizungumza katika mkutano huo, Kazura alielezea wasiwasi wake juu ya vitisho vinavyoendelea vinavyozikabiliwa nchi hizo mbili ambazo alisema zinahitaji juhudi za pamoja kuzishughulikia.

Beya kwa upande wake alisisitiza utayari wa nchi yake kushirikiana na Rwanda katika harakati za usalama.

Chanzo: HabariLeo