0

Miss aenguliwa urais Uganda

Thu, 5 Nov 2020 Source: habarileo.co.tz

MWANDISHI wa habari wa zamani na mshiriki wa Miss Uganda, Nancy Linda Kalembe ameondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa nchi hiyo kama mgombea huru.

Kalembe kama angefanikiwa kuwania nafasi hiyo angekuwa mgombea pekee wa kike katika mbio hizo zinazoshirikisha wagombea 11.

Tume ya Uchaguzi ya Uganda juzi ilimuondoa Kalemba baada ya kushindwa kuwasilisha ada ya Sh milioni 20 ya kuteuliwa katika nafasi hiyo.

Kalembe ambaye aliwasilisha fomu zake katika Tume hiyo alitakiwa kurekebisha kasoro katika fomu zake na kurudi tena Jumanne ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha fomu hizo pamoja na fedha.

“Umeshindwa kuendana na kanuni zilizowekwa ambazo zinakutaka kuwasilisha kiasi cha Sh milioni 20 kabla ya kutaka uteuzi. Hivyo hatutaweza kukuteua wewe kwa sababu haujakamilisha vigezo vilivyowekwa. Hivyo tafadhali wakala wako waje kwa ajili ya fomu zako,” alisema Mwanasheria wa Tume hiyo, Simon Byabakama Mugenyi.

Chanzo: habarileo.co.tz