0

Miss Morgan: Maisha Yalimswaga na Kufanya Awe Mama Pewa

Thu, 25 Mar 2021 Source: kiswahili.tuko.co.ke

- Waliokuwa waigizaji wa kipindi cha Tahidi High wanajitokeza na kusimulia masaibu wanayopitia maishani

- Kwa muda, walikuwa ndio nyuso za kutamaniwa lakini kile mashabiki hawakujua ni kuwa baadaye nyuso hizo zilipata masaibu mengi

- Miss Morgan alisema aliingilia ulevi na isipokuwa ni marafiki na familia chupa ingemteka kabisa

Aliyekuwa muigizaji wa kipindi cha Tahidi High Angel Waruinge almaarufu Miss Morgan amesimulia masaibu yaliyompata baada ya kibarua kutamatika katika runinga.

Miss Morgan alisema kipindi hicho kilifika tamati na waliokuwa waigizaji kulazimika kutafuta njia mbadala za kujichumia riziki.

Kwenye mahojiano katika Youtube, Miss Morgan alifungua roho kuhusu alivyogeuka na kuwa mlevi kupindukia.

"Unapoanza kuishi maisha yasiyo yako unazongwa na mawazo sana. Nilipitia masaibu ya kuzongwa na mawazo . . . Na mawazo kupita kiasi yanaweza kukufanya uingilie kileo. Nilianza kulewa na nilibahatika tu kwa kuwa na familia na marafiki wazuri ambao waligundua masaibu yangu," alisema Miss Morgan.

Alisimulia pia masaibu ambayo yanawapata wasanii humu nchini akisema wao hulazimika kuishi maisha ambayo hawawezi kuyagharamia.

"Unapoanza kuwa maarufu, huwa unaanza maisha mengine na hapo kuanza kukosa fedha lakini bado unataka kuishi maisha ya juu. Hapo ndio unaishi maisha ya kuwafurahisha watu," alisema.

Waruinge, ambaye ni mama ya mtoto mmoja msichana, alikuwa miongoni mwa talanta maarufu katika kipindi hicho cha Tahidi High.

Alisema alilazimika kuhama maeneo aliyokuwa akiishi ili kubadili maisha aliyokuwa ameingilia.

Simulizi za msanii huyo zinafuata za wenzake kwenye kipindi hicho Dennis Mugo almaarufu OJ na Joseph Kinuthia akijulikana sana kwa jina Omosh.

OJ aliingilia raha za kileo kiasi cha kuishia katika kituo cha kurekebisha tabia ya uzoefu wa mwili kwa vileo.

Kwa sasa Omosh anajengewa nyumba na wahisani baada ya kulia mtandao akiomba Wakenya kumsaidia maisha yalipomkaba koo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.

Chanzo: kiswahili.tuko.co.ke