0

Magufuli asimamisha shughuli ya Tanasha

Thu, 25 Mar 2021 Source: www.habarileo.co.tz

STAA wa muziki raia wa Kenya, Tanasha Donna ameamua kuahirisha kitu alichotaka kuwaachia mashabiki wake kupisha kipindi cha maombolezo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli aliyefariki Machi 17, mwaka huu.

Tanasha ambaye ni mzazi mwenza na staa wa muziki wa Bongo Flava, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameamua kufanya hivyo kama heshima yake kwa Rais Magufuli ambaye aligusa watu wengi kutokana na utendaji wake.

Nyota huyo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram “Niliwaahidi mashabiki wangu kuwa kesho (leo) nilitaka kuwashangaza, lakini kwa heshima siwezi kufanya hivyo katika kipindi hiki ambacho tumempoteza kiongozi bora Afrika.”

“Tumeamua kuisogeza mbele siku hiyo hadi wakati mwingine tuendelee kuwa na subira ,” alisema Tanasha ambaye hivi sasa amekuwa akifanya kazi nzuri katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Kitendo hicho kimewagusa mashabiki wengi ambao wamefurahishwa na msanii huyo kumthamini Rais Magufuli ambaye alikuwa kipenzi cha wengi sio kwa Watanzania pekee bali bara zima la Afrika na dunia nzima kutokana na misimamo yake pamoja na kujitoa kwa wengine.

Chanzo: www.habarileo.co.tz