0

Lampard amvutia kasi Zaha

Thu, 2 Jan 2020 Source: mwananchi.co.tz

London, England. Frank Lampard ameahidi kufanya usajili bora katika kikosi hicho kulingana na mahitaji ya timu wakati huu wa dirisha la usajili.

Kocha huyo wa Chelsea amewaweka katika rada yake wachezaji wanne anaotaka saini zao Wilfried Zaha, Jadon Sancho, Moussa Dembele na Nathan Ake.

Klabu hiyo imeruhusiwa kusajili baada ya kuondolewa kifungo na Lampard anataka kuongeza mastaa wenye uzoefu wa kutosha katika mashindano.

Lampard amesema anataka kusajili wachezaji ambao wataendana na falsafa yake katika kikosi hicho ili wawe na manufaa kwa klabu.

Wakati dirisha la usajili lilifunguliwa jana, wachezaji watatu akiwemo mshambuliaji nguli Olivier Giroud, Pedro na Willian watakuwa nje ya mkataba katika majira ya kiangazi.

Zaha na Sancho wanapewa nafasi na Lampard lakini Dembele amekuwa akihusishwa muda mrefu na klabu hiyo ya Stamford Bridge tangu akiwa Fulham.

Pia Lampard anataka beki wa kushoto na jicho limetua kwa mchezaji wa Bournemouth Ake ambaye amekuwa katika kiwango bora msimu huu.

Kocha huyo alisema wanaendelea kufanya tathimini kuangalia namna bora ya kuboresha kikosi hicho katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu.

Chanzo: mwananchi.co.tz