0

Koffi Olomide: Natetemeka kwa furaha, nitafanya makubwa

Fri, 6 Mar 2020 Source: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Antoine Christophe Agbepa Mumba maarufu Koffi Olomide, mwanamuziki wa rhumba ameahidi kufanya makubwa katika onyesho lake linalofanyika kesho Jumamosi Machi 7,2020 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Koffi aliyezaliwa mwaka 1956 ambaye anatamba na wimbo wa Papa Ngwasuma kwa sasa amewaeleza waandishi wa habari leo Ijumaa Machi 6, 2020 kuwa amekuja Tanzania  na nguvu ya ajabu, lengo likiwa kuwapa burudani watakaohudhuria onyesho hilo.

Huku akizitaja baadhi ya nyimbo atakazoimba, Micko, Selfie, Ultimatum, Abracadabra amesema, “Tanzania ni kati ya nchi ninazozipenda, najisikia faraja moyo wangu unatetemeka kwa furaha hivyo watu wategemee burudani kutoka kwangu.”

Alipoulizwa siri ya kuendelea kutumbuiza hadi sasa licha ya umri kuelekea kumtupa mkono amesema anapenda tasnia ya muziki, kujituma na kuwataka wanaopenda muziki kuiga mfano wake.

Chanzo: mwananchi.co.tz