0

Kina Gigy Money wamponza Erick Omondi

Fri, 12 Mar 2021 Source: www.mwanaspoti.co.tz

By Kelvin KagamboMore by this Author Polisi nchini Kenya wamemkamata mchekeshaji Eric Omondi leo Machi 11 kwa kosa la kusambaza tamthilia yake ya Wife Material bila kibali, tamthilia ambayo msanii wa muziki wa Tanzania Gift Stanford maarufu Gigy Money ameigiza pia.

Mkuregenzi wa Bodi ya Filamu Kenya, Ezekiel Mutua amethibitisha kukamatwa kwa Omondi na kueleza kuwa amekiuka sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaani ya Mwaka 1998 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

“Sheria ya Kenya inasema mtu yeyote hataruhusiwa kuonyesha filamu kwenye onyesho lolote au kuisambaza filamu ikiwa hana kibali kutoka bodi kinachothibitisha kuwa yeye ni muonyeshaji au msambazaji wa filamu.” alisema Mutua.

Tamthilia hiyo ambayo ni ‘reality show’ iliyoanza kutengenezwa mapema wiki jana ikiwa ni msimu wa pili inamulika tabia mbali mbali za wanawake wa kisasa wa Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja wanavyowahudumia wapenzi wao. Ambapo tamthilia nzima imekusanya wanawake maarufu kutoka Kenya, Uganda na Tanzania wakielezea tabia hizo pia kuzionyesha kwa vitendo.

Hata hivyo mara tu baada ya kuachiwa kwa vipande vya video vya sehemu ya kwanza ya msimu wa pili wa tamthilia hiyo maoni ya watazamaji kadhaa mtandaoni yameonyesha kuchukizwa na dhamira ya tamthilia nzima kwa madai kwamba imejaa picha za zisizorandana na maadili ya kiafrika na zinazodhalilisha wanawake.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz