0

Kampuni yaleta neema kwa wanamuziki Afrika Mashariki

Kampuni yaleta neema kwa wanamuziki Afrika Mashariki

Sun, 7 Mar 2021 Source: HabariLeo

KAMPUNI inayoongoza katika usambazaji wa muziki kidijitali na kukusanya mirabaha ya wasanii huru ya TuneCore imezindua shughuli zake rasmi Afrika Mashariki na barani Afrika kwa jumla.

Jade Leaf, Mkuu wa TuneCore ya Afrika ya Kusini anasema atashiriki kwenye majukumu katika nchi za Afrika Mashariki akiwa sambamba na Chioma Onuchukwu, ambaye ni Mkuu wa TuneCore Afrika Magharibi.

Leaf na Onuchukwu wanafanya kazi hiyo huku wakiripoti kwa Faryal Khan-Thompson, Makamu wa Rais wa Kimataifa wa TuneCore.

Taarifa iliyotolewa na Thompson inaonesha kwamba Onuchukwu atakuwa Nigeria na kwamba atasimamia nchi za Afrika Magharibi ikiwemo Nigeria, Ghana, Liberia, Siera Leon na Gambia.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Onuchukwu pia atasimamia kazi wasanii Tanzania na Ethiopia.

Himaya ya Leaf katika kusambaza muziki wa wasanii na kusimamia mirabaha inajumuisha nchi za eneo la kusini mwa Afrika za Namibia, Botswana, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Lesotho na Afrika Kusini ambako ndiko makao makuu.

Leaf yeye, taarifa inasema, atasimamia pia shughuli za TuneCore katika nchi za Afrika Mashariki, Kenya na Uganda.

“Ninafuraha kuwa ninajiunga na kampuni huru maarufu ya usambazaji wa muziki, hasa katika karne hii adhimu kwa wabunifu wa muziki barani Afrika wakati ambao tunapata kutambuliwa kimataifa na tunaongezea bidii,” taarifa imemkariri Onuchukwu akisema.

"Ninatazamia kushirikiana na kuwaunga mkono wasanii wa nchi hizi ninazozisimamia,” aneongeza.

Kabla ya kujiunga na TuneCore, Onuchukwu alikuwa Meneja wa Masoko katika kampuni ya uduX Music ambayo ni jukwaa la kutiririsha muziki nchini Nigeria.

Alifanya kazi katikia jukwaa hilo pamoja na wasanii maarufu wa Afrika kama vile Davido, Yemi Alade, Patoranking, Kizz Daniel na wengine wengi.

Kwa upande wake, Leaf amekaririwa akisema: “Ninafuraha sana kujiunga na timu hii wakati ambao mazungumzo ya kimataifa yanahusu uhuru na umiliki."

Awali, Leaf alifanya kazi katika moja ya kampuni kubwa ya televisheni Afrika ya Multichoice kama Meneja wa Masoko wa Vituo vya Vijana na Muziki, ambapo aliongoza katika kuipa kampuni hiyo sura mpya hususani kupitia kituo kikubwa cha Muziki wa TV cha Channel O.

Kabla ya hapo alifanya kazi na kampuni ya Sony Music Entertainment Africa, akilenga wasanii na maudhui ya Kiafrika. Alihusika pia na kampeni nyingi za masoko na miradi ya wasanii kimataifa.

TuneCore inafungua ulimwengu wa uwezo kwa wasanii huru katika kila ngazi ya kazi zao.

Afrika ni makao ya wasanii mbalimbali wanaotafuta huduma thabiti ya usambazaji wa kazi zao na kampuni hii imeonesha inaelewa mahitaji yao na inaweza kuwapa nafasi ya kubadilisha sanaa yao kuwa yenye ufanisi wa kibiashara.

Katika mwaka wa 2020, TuneCore ilishuhudia ongezeko katika matoleo ya muziki kimataifa, huku wasanii wengi wa Kiafrika wakichagua kutumia wasambazaji wa DIY - DJ Spinall na Small Doctor nchini Nigeria, Spoegwolf nchini Afrika Kusini, Mpho Sebina nchini Botswana na Fena Gitu nchini Kenya.

“Afrika ni soko linalosisimua sana la muziki lenye uwezo mkubwa wa kukua," amesema bosi wa TuneCore, Thompson katika taarifa.

TuneCore, inayomilikiwa na Believe ya Paris, imekuwa ikipanua kwa haraka shughuli zake za kimataifa, kuanzia nchi tano mwaka wa 2020 hadi nchi nane na maeneo matatu makuu ya dunia mwaka huu wa 2021.

Katika mwaka uliopita, kampuni hii ilizidi pia kujitanua hadi India, Urusi na Brazili, Asia ya Kusini Mashariki na sasa Afrika.

Chanzo: HabariLeo