0

Wakongo ‘waipa tano’ serikali

18a0222e9157c1d2e2bb6b4a535cf916 Wakongo ‘waipa tano’ serikali

Thu, 8 Apr 2021 Source: www.habarileo.co.tz

UMOJA wa wafanyabiashara kutoka nchini Kongo ujulikanao kwa jina la Business Congolese International (BCI), umeipongeza serikali kwa kuliangalizia suala la kodi kwa wafanyabiashara na kudai kuwa hatua hiyo ni njema katika kuamsha upya hali ya wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Wakizungumza mkoani Dar es Salaam, viongozi wa umoja huo walisema kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka suala la kodi kwa wafanyabiashara liangaliwe kwa umakini, imewafurahisha na kuwarejeshea matumaini upya.

Walisema malengo ya wafanyabishara ni kufanya biashara katika mazingira rafiki ili wapate faida na kutimiza jukumu lao la kulipa kodi kwa serikali kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Makamu Mwenyekiti wa BCI, John Kapeta alisema kauli ya Rais Samia kuhusu makusanyo ya kodi kwa wafanyabiashara na msisitizo uliotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango sambamba na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ni mambo yaliyowapa matumaini makubwa katika shughuli zao za kibiashara.

"Kweli tumefarijika na kauli ya Rais Samia kuhusu suala la kodi, unapomlinda mfanyabiashara unasaidia kulinda uchumi wa nchi, nasi kwa umoja wetu kama wafanyabiashara kutoka nchini Kongo, tunamuahidi kuendelea kumpa ushirikiano wa hali ya juu," alisema Kapeta.

Alisema wanaahidi kupeleka salamu hizo kwa wafanyabiashara waliopo Congo ili kuwavutia kuja nchini kuwekeza na kufanya biashara.

Rais wa BCI, Mukendi Godefroid, alisema kitendo cha uongozi mpya wa nchi kukumbuka mazingira ya wafanyabiashara, kimewapa faraja.

Alisema wataendelea kushirikiana na mamlaka zote za serikali ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutekeleza masuala yanayohusu uingizaji na usafirishaji wa mizigo na mambo mengine ya kibiashara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz