0

Chuchu Hans, Patcho Mwamba ndani ya filamu moja na Awilo Longomba

Chuchu Hans, Patcho Mwamba ndani ya filamu moja na Awilo Longomba

Fri, 9 Apr 2021 Source: Mwanaspoti

Wasanii wa filamu nchini Tanzania, Chuchu Hans na Patcho Mwamba wanatarajiwa kuonekana katika filamu moja na Mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Awilo Longomba.

Hayo yameelezwa jana Aprili 8, 2021 na muandaaji wa filimau hiyo, Leo Brown,wakati wa mapokezi ya mwanamuziki huyo katika uwanja wa Mwalimu Nyerere,jijini Dar es Salaam.

Brown amesema filamu hiyo itakayoitwa 'A life to Regret', itashirikisha wasanii wa nchi mbalimbali wakiwemo hao wa Tanzania Chuchu na Patcho.

Akieleza sababu ya kumshirikisha Longomba, Brown amesema ni katika kuchanganya ladha ya wasanii wa filamu na muziki na kuleta kitu tofauti katika tasniia hiyo.

"Katika utengenezaji filamu lazima uwe mbunifu ikiwemo kuchanganya watu wanaofanya kazi tofauti,ndio maana katika filamu hii tumeona tumuweke na Longomba ambaye ana mashabiki wengi Afrika na nje ya bara la Afrika kupitia muziki," amesema.

 Kwa upande wake Longomba amesema amejisikia furaha kuonekana moja ya wanamuziki wanaoweza kushiriki katika filamu na kueleza kuwa hii ndio mara yake ya kwanza kucheza filamu.

"Kuna wanamuziki wengi ambao Brown angeweza kuwachukua,lakini aliniona mimi kati ya hao namshukuru kwa kunithamini na ninaahidi sitamuangusha," amesema.

Wakati kuhusu kuja Tanzania emesema amefurahi ukizingatia kwamba ni takribani miaka 20 imepita tangu alipokuja kufanya show na kueleza ni nchi ambayo anaipenda kutokana na kupenda muziki wake na kuchangia umaarufu wake.

Wasanii wengine watakaokuwepo ndani ya filamu hiyo ni Jackie Musunga wa Marekani na mchekeshaji Mai Tt Dairies maarufu kwa jina la Matiti wa nchini Zimbabwe.

Chanzo: Mwanaspoti