0

Chamileon amuaga  Magufuli Dodoma

Tue, 23 Mar 2021 Source: www.habarileo.co.tz

STAA wa muziki kutoka nchini Uganda, Joseph Mayanja maarufu Jose Chameleone jana aliungana na mamia ya Watanzania mkoani Dodoma kumuaga aliyekuwa Rais wa Tano, Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 Dar es Salaam.

Chamileon aliambatana na msanii mwingine kutoka nchini Uganda, Pius Mayanja ‘Pallaso Music’ ambaye aliwahi kushiriki katika tuzo za MTV.

Chamileon, ambaye aliwahi kutamba na albamu kama vile Mama Mia, Mambo Bado, Jamila, Kipepeo, Bageya, Shida za Dunia, Bayuda na Njoo Karibu, ni miongoni mwa wasanii wenye majina makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na kazi zake nzuri.

“Hii inaonyesha wazi jinsi gani Magufuli alikuwa akigusa maisha ya wengi kutokana na utendaji kazi wake enzi za uhai wake hakika taifa limepoteza moja ya nguzo kuu katika muhimili wake.”

Chameleon aliandika hayo jana katika ukurasa wake wa Instagram alipokuwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA) akiwa njiani kwenda Dodoma:

“Ndugu zangu wabongo poleni sana kwa msiba mkubwa wa Rais mpenda wanyonge, hili ni pigo kubwa ila Mungu atatuvusha.”

“Mimi na Ndugu yangu Pallasomusic tunawakilisha tunaungana nanyi kumuuaga Rais Magufuli. Mungu ametoa, Mungu ametwaa jina lake lihimidiwe, amen” aliandika Chameleon.

Chanzo: www.habarileo.co.tz