0

Buriani Aurlus Mabele, gwiji wa Soukous

Thu, 26 Mar 2020 Source: mwananchi.co.tz

Usiku wa Alhamisi na hata asubuhi ya Ijumaa imekuwa ngumu mno kwa mashabiki wa muziki wa Lingala, hususani Soukous. Hii ni kutokana na taarifa za kufariki dunia kwa gwiji wa miondoko hiyo, Aurlus Mabele.

Mabele aliyewahi kutamba na makundi mbalimbali ya muziki nchini Kongo - Brazzaville alikozaliwa na ile ya DR Congo, inaelezwa amekumbwa na mauti akiwa Ufaransa usiku wa kuamkia jana kwa kilichoelezwa sababu ya virusi vya corona.

Bintiye nyota huyo wa zamani wa Loketo Group, Liza Monet alithibitisha taarifa za kifo cha mzazi wake kupitia akaunti yake ya Facebook kwamba, amekufa kutokana na Covid19, sawa na alivyofanya mpwawe, Robert Mabele aliyekiri mjomba wake amefariki Alhamisi.

Kabla ya kukumbwa na mauti, Mabele alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya muda mrefu yaliyomuweka kitandani ikiwamo saratani ya koo miaka kadhaa nyuma sambamba na kupooza. Mashabiki na wasanii mbalimbali waliowahi kufanya kazi na mwimbaji huyo aliyekuwa mahiri pia kwa kutunga na kucheza, wametoa salama za rambirambi juu ya kifo chake.

Mabele ni nani?

Mashabiki wa muziki wa Kikongo walimfahamukupitia Kundi la Loketo (Loketo Group), lililojumuisha magwiji na nyota mbalimbali wa muziki barani Afrika na hasa kutoka nchi za DR Congo na Kongo -Brazzaville.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Ila ukweli Mabele ambaye majina yake halisi ni Aurelien Miatsonama, alianza kufahamika tangu akiwa kwao Kongo - Brazzaville kupitia kundi la Ndimbola Lokole lililoasisiwa mwaka 1974 akiwa sambamba na kina Jean Baron, Pedro Wapechkado na wengine, na miaka michache baadaye ndipo walipolianzisha kundi la Loketo.

Mtunzi na mwimbaji huyo aliyekuwa mahiri pia kwa kunengua jukwaani alizaliwa 1953 katika Wilaya ya Poto-Poto, iliyopo jijini Brazzaville.

Historia ya maisha yake ya utotoni haitajwi sana, lakini kama ilivyo kwa wanamuziki wengi alianza sanaa tangu akiwa mdogo kupitia makundi kadhaa ya mitaani yaliyompa uzoefu.

Inaelezwa kuwa kabla ya kugeukia utunzi na uimbaji, Mabele alikuwa akidansi, lakini kwa kuwa alikuwa na kipaji cha muziki ilikuwa bahati kwake kubadilisha upepo mapema.

Safari yake kimuziki na kuanza kwake kufahamika ilianza rasmi miaka ya 1970 wakati alipoungana na wanamuziki wenzake May Cacharel, Jean Baron, Pedro Wapechkado na wengine walioasisi Ndimbola Lokole mwaka 1974.

Kundi hilo lilijipatia umaarufu mkubwa kutokana na ziara za mara kwa mara barani Ulaya kabla ya baadaye, yeye na Jean Baron ambaye pia ni marehemu kwa sasa walipoungana na nyota kutoka DR Congo enzi hizo (Zaire) na kuunda kundi la Loketo.

Kundi hilo liliasisiwa mwaka 1987 na Mabele mwenyewe, Diblo Dibala, Jean Baron, May Cacharel walikuja kuungana na wakali kama Fred Mayunga, Lucien Bokilo, Mack Mackaire, Jean Bilongo, Komba Bello Mafwala na Awilo Longomba alipiga tumba.

Ufalme wa Soukous

Uimbaji na ucheshi wake jukwaani sambamba na kipaji chake cha kuburudisha vilimfanya Mabele kupewa jina la Mfalme wa Soukous ambayo ilikuja kuzaa albamu yenye jina kama hilo la King Of Soukous (Soukous la Terreur iliyotoka kati ya mwaka 1989 na 1991).

Sura yake iliyokuwa imejaa tabasamu muda wote ilimfanya Mabele awe kipenzi cha mashabiki wengi hasa wa kike, uvaaji na uchezaji wake vilimtofautisha na wanamuziki wengine miaka hiyo. Nyimbo kama Asta de, Zebola, Ebouka, Wakawaka, Liste Rouge, Zenab, Mawa, Evelyne, Generation Wachiwa, Betty, Femme Ivoirienne, Rosine, Mali Bamako, Doce Isabelle, Keba, Soukous Trouble, Loketo, Khadydja, Rosa, Embargo, Stop Arretez na nyinginezo zilimbeba na kumtangaza duniani.

Ziara ndefu aliyofanya na Loketo Group barani Ulaya ilimtangaza na wenzake na hasa kupitia albamu yao ya Extra Ball na haikuwa ajabu baadhi yao kulowea barani humo.

Mabele na kina Diblo waliweka maskani yao Ufaransa na wengine kukimbilia Ubelgiji, na kuna wengine walienda kuweka maskani yao Marekani.

Hawa ni wale waliojitoa Loketo na kwenda Soukous Stars ya kina Yondo Sister, Shimita, Lokasa ya Mbongou, Ngouma Lokito na wengineo.

Kuishi kwake Ufaransa kunaelezwa kulimsaidia kupata mtoto wa kike anayetambuliwa zaidi na mashabiki wake, Liza Monet.

Mwanadada huyo ambaye naye ni mwamuziki kwa sasa anaishi Ufaransa na anaelezwa ndiye anayejulikana zaidi kuliko watoto wengine ambao mwanamuziki huyo amejaliwa kuzaa.

Kavuna fedha za kutosha

Inaelezwa kuwa kwa miaka zaidi ya 25 ya kudumu kwake kwenye muziki, Mabele aliuza nakala zaidi ya milioni 10 na kuvuna fedha za kutosha zilizomfanya aishi kitajiri.

Watayarishaji wakubwa wa muziki aliofanya nao kazi na kumtengenezea njia ya kuvuna fedha kupitia albamu na nyimbo zake ni pamoja na Jimmy Houtienou kupitia Jimmy’s Production, AJIP Production, Afro Rythmes, JPS, Jip Records na wengine. Ukiacha albamu ya Soukous la Terreur, albamu ya Stop Arretez ndiyo iliyompa fedha nyingi zaidi ikifuatiwa na ile na Toure de Controle.

Baadhi ya albamu zilizomtangaza Mabele ni pamoja na albamu kama Soukous la Terreur (1991), Stop Arretez (1993), Tour de Controle (1999), Dossier X (2000) na Fiesta d’Or aliyoifyatua mwaka 2002.

Alitibuana na Diblo

Licha ya kupata mafanikio makubwa wakiwa pamoja, Mabele na Diblo walitengana ndani ya muda mfupi mwishoni mwa mwaka 1990, japokuwa walikuja baadaye kushirikiana tena kufanya kazi binafsi. Inadaiwa Diblo hakupendezwa na tabia alizokuwa nazo Mabele ikiwamo ya kutembea na wanenguaji wao na kufikia hatua ya kuwapa nafasi kubwa kundini kiasi cha kuwashirikisha kuimba nyimbo zao.

Maradhi yamtesa

Miaka michache iliyopita, Mabele aliwahi kuhojiwa akiwa nchini Ufaransa alikopelekwa kwa matibabu na kueleza kuwa anaumizwa zaidi baada ya aliyekuwa mkewe kumtelekeza hospitali.

Inadaiwa tatizo kubwa lililomsumbua mwanamuziki huyo mahiri ni maradhi ya kansa ya koo yaliyoelezwa kumfanya ashindwe kuzungumza vizuri.

Kipindi akiendelea kujiuguza ilikuwa vigumu kujua Mabele amelazwa hospitali gani kutokana na uwapo wa taarifa mbili tofauti, moja ikielezwa yupo visiwa vya West Indies, Carribean na wengine wakidai yupo Ufaransa akiuguzwa na baadhi ya marafiki zake.

Rafiki zake hao walikuwa wakiendesha harambee kupitia mtoto wa mtayarishaji wake mahiri wa muziki, Jimmy Houtienou na huku wakiendelea kuwaomba mashabiki waendelee kumuombea.

Inaumiza, ila ukweli ndiyo huo gwiji na mfalme huyo wa Soukous kwa sasa hatunaye tena duniani kwa vile ameshaumaliza mwendo. Kwa hakika kila nafsi itaonja mauti. Tangulia Mabele...tangulia gwiji wa miondoko ya Soukous.

Chanzo: mwananchi.co.tz