0

Akon azuru Uganda kibiashara

Sun, 4 Apr 2021 Source: www.habarileo.co.tz

MWANAMUZIKI Aliaune Damala Badara Thiam, ‘Akon’ amewasili Uganda kwa ziara ya kibiashara.

Akon mzaliwa Senegal ambaye pia ni raia wa Marekani amekwenda Uganda baada ya hivi karibuni mkewe, Rozina Negusir kuzuru nchi hiyo pia.

Negusir alikutana na Rais Museveni na wakajadili miradi tofauti ya uwekezaji ambayo inaweza kufanywa, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje.

Akon alipokelewa na Abbey Walusimbi, mshauri mwandamizi wa Rais katika masuala ya raia walio nje ya nchi hiyo, mwanamuziki Eddie Kenzo, maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bodi ya Utalii ya Uganda, na Shehe Ramadhan Mulindwa kutoka Baraza Kuu la Waislamu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, katika ziara yake Akon pia anatarajiwa kukutana na Rais Yowel Museveni kujadili fursa tofauti za uwekezaji katika sekta mbalimbali za nishati, utalii, maendeleo ya miundombinu na nyinginezo.

Mwaka 2018 Akon alitangaza mpango wa kujenga jiji la kisasa kwa Dola za Marekani bilioni 6 nchini Senegal kwa jina “Akon City”.

Mradi huo unaoungwa mkono na Serikali ya Senegal utakuwa na hoteli za kifahari, studio za muziki, maduka makubwa ya bidhaa na vivutio vingine.

Chanzo: www.habarileo.co.tz