0

Zverev atinga nusu fainali US Open

Zverev atinga nusu fainali US Open

Thu, 10 Sep 2020 Source: HabariLeo

MJERUMANI anayeshika nafasi ya tano kwa ubora katika mchezo wa tenisi, Alexander Zverev, amepambana kutoka nyuma na kutinga kwa mara ya kwanza nusu fainali ya mashindano ya US Open, akimshinda, Borna Coric.

Zverev, 23, alijikuta akichapwa katika seti ya kwanza wakati Mcroatia anayeshikilia nafasi ya 27 akijipa matumaini ya kushinda taji lake la kwanza kubwa.

Lakini katika seti mbili zilizofuata, Zvarev alifanya kweli na kushinda zote, ambapo katika seti ya nne Mjerumani huyo alishinda 1-6 7-6 (7-5) 7-6 (7-1) 6-3.

“Nilianza kucheza vizuri kidogo. Jinsi nilivyokuwa nacheza sio kiwango kile ambacho kinatakiwa kuchezwa katika hatua ya robo fainali ya mashindano makubwa kama US Open.

Sitaki kuishia hapa,” alisema Zverev baada ya mchezo huo. Kwa ushindi huo, Zverev sasa atacheza dhidi ta Mhispania anayeshikilia nafasi ya 20, Pablo Carreno Busta, ambaye alimfunga Mcanada anayeshikilia nafasi ya 12 kwa ubora, Denis Shapovalov kwa 3-6 7-6 (7-5) 7-6 (7-4) 0-6 6-3 katika mchezo uliodumu kwa zaidi ya saa nne.

Carreno Busta, 29, ambaye pia alicheza hatua ya nne bora katika mashindano ya mwaka 2017, alisema: “Nimepambana, lakini nina furaha kubwa. Baada ya mpambano huu mgumu nimefurahi tena kutinga nusu fainali.”

Bila kuwepo akina Roger Federer na Rafael Nadal, pamoja na uamuzi wa kumuondoa Novak Djokovic katika mashindano Jumapili, bila shaka sasa kutakuwa na bingwa mpya wa mashindano ya mwaka huu ya US Open.

Kwa upande wa wanawake, Naomi Osaka, anayeshika nafasi ya nne kwa ubora ametinga nusu fainali ya mashindano ya US Open, baada ya kumchapa bingwa namba 93 kwa ubora, Shelby Rogers, kwa seti tatu mfululizo.

Mmarekani Rogers, mwenye umri wa miaka 27, alimshangaza Petra Kvitova anayeshikilia nafasi ya nne, lakini alishindwa kuendana na kasi ya bingwa huyo wa mwaka 2018.

Chanzo: HabariLeo