0

Yanga yamsimamisha katibu mkuu wake

Yanga yamsimamisha katibu mkuu wake

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

IKIWA ni siku chache zimepita tangu kuibuka kwa tuhuma dhidi ya Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Wakili Simon Patrick kuwa anavujisha siri za klabu, Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo imemsimamisha kazi.

Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa jana na Mwenyekiti wake, Dk Mshindo Msolla, uamuzi huo umekuja baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kilichokaa juzi maalum kwa ajili ya kusikiliza tuhuma ambazo kiongozi huyo amehusishwa nazo.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo alimtuhumu Patrick ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama kuwa alikuwa na vikao vya siri na kiongozi wa mahasimu wao, anahofia nafasi yake isichukuliwe na mshauri wa klabu hiyo Senzo Mbatha na kwamba pia amehujumu kesi ya Bernard Morrison.

Hata hivyo, kabla ya taarifa hiyo ya kusimamishwa kazi, juzi Patrick kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram alifafanua tuhuma hizo, kwanza akikiri kuwa alikutana na Mtendaji wa mahasimu wao katika klabu ya Yatch lakini sio kwa ajili ya kutoa siri bali kuna mambo muhimu alikuwa anafuatilia na viongozi wa Yanga wanajua.

Alisema pia hamhofii Senzo kama ilivyodaiwa kwa kuwa sio mwanasheria kama yeye na wako katika nafasi tofauti.

Pia alisema yeye hajahujumu kesi ya Morrison kwani hakufudhu kutetea kesi hiyo na ndio maana klabu iliamua kuweka wanasheria.

Chanzo: HabariLeo