0

Yanga tayari kuikabili Prisons

Thu, 3 Sep 2020 Source: habarileo.co.tz

YANGA wanaendekea na maandalizi makali kwa ajili ya ufunguzi wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons itakayofanyika Jumapili, jijini Dar es Salaam.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema jana kuwa, mazoezi yanaendelea vizuri chini ya Kocha Mkuu, Zlatko Krmpotic na kwamba kwa sasa wanakazania kutengeneza muunganiko wa timu.

“Mazoezi yanaendelea vizuri na wachezaji wanafanya kile wanachoelekezwa na walimu wao tayari kuanza mchakamchaka wa kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema.

Mwambusi alisema mazoezi hayo yaliyoanza hivi karibuni kwa sasa yanahudhuria na wachezajji karibu wote na kila kitu kinaenda sawa.

Akizungumzia kuhusu majeruhi katika timu hiyo ambayo msimu huu imepania kumaliza ukame wa mataji baada ya kukosa mataji kwa msimu mitatu mfululizo, alisema Balama Mapinduzi ndio majeruhi pekee aliyekuwepo, huku Andulaziz Makale amepona na anaendelea vizuri.

Yanga Jumapili iliyopita ilihitimisha Wiki ya Mwananchi, ambapo ilivunja rekodi kwa kuujaza Uwanja wa Mkapa na kutuma salama kwa wapinzani wao, hasa Simba ambao kwa muda mrefu walikuwa wakitamba kuwa wao pekee ndio wenye uwezo wa kuujaza uwanja huo.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga watakaoonekana msimu huu ni makipa, Metacha Mnata, Farouk Shikhalo na Ramadhan Kabwili, wakati mabeki ni Paul Godfrey, Kibwana Shomari, Yasin Mustafa, Adeyun Saleh, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Said Makapu na Abdallah Shaibu.

Wachezaji wa viungo ni Mukoko Tonombe, Zawadi Mauya, Abdulaziz Makame ‘Bui’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Haruna Niyonzima, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke, Juma Mahadhi, Farid Mussa, Tuisila Kisinda na Carlos Carlinhos.

Wakati washambuliaji ni Adam Kiondo, Ditram Nchimbi, Wazir Junior, Yacouba Songne na Michael Sarpong.

Chanzo: habarileo.co.tz