0

Wadau wa netiboli wamzika Anna Kibira

Wadau wa netiboli wamzika Anna Kibira

Tue, 8 Sep 2020 Source: Mwanaspoti

By Imani MakongoroDar es Salaam. Makocha, waamuzi na baadhi ya wachezaji wa netiboli nchini wameeleza mchango wa Anna Kibira katika maisha yao na namna alivyowajenga kwenye mchezo huo.

Kibira aliyewahi kuwa mchezaji, kocha, mkufunzi, katibu mkuu na mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) alifariki Septemba 4 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Wakizungumza wakati wa ibada ya kuaga mwili kwenye kanisa la KKKT Keko, Dar es Salaam, jana, wadau hao wa netiboli kwa nyakati tofauti walielezea mchango wa Kibira kwenye netiboli.

“Ndiye aliyekuwa mkufunzi wangu wa kwanza nilipoingia kwenye ukocha 1999, dada Anna ametuachia pigo kwenye netiboli,” alisema Amina Mussa, mwamuzi wa netiboli nchini.

Matalena Mhagama alimtaja Kibira kuwa kocha, ambaye alimuibua na kumtaka apambane ili kufikia mafanikio.

Kocha wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Queens), Winfrida Emmanuel alisema Kibira alijitolea maisha yake yote kwenye netiboli.

Chanzo: Mwanaspoti