0

Wadau Stars watoa ya moyoni

Wadau Stars watoa ya moyoni

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

WADAU mbalimbali wa soka nchini wametoa maoni yao kuhusu timu ya taifa, Taifa Stars, wakisema bado ina nafasi ya kufuzu fainali za Afrika (Afcon) ila umakini unahitajika zaidi.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, walisema kuna mapungufu mengi yameonekana katika mchezo uliopita dhidi ya Tunisia lakini yakifanyiwa kazi timu inaweza kufanya vizuri michezo inayokuja na kufuzu kucheza fainali hizo.

Mmoja wa wadau hao ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mustapha Hoza alisema nafasi ipo na kinachotakiwa kufanyiwa kazi kwa sasa na kusahihisha makosa ili timu iweze kuwa bora na kujiamini zaidi.

“Ukitizama michezo miwili iliyopita dhidi ya Tunisia hatukujiamini ndio maana tulikuwa tunapoteza mipira hatukai nayo, umakini haukuwapo tulikuwa tunaonekana kama watu wanaojifunza.”

“Mechi kubwa kama hizo kwa maana ya kimashindano zinahitaji wachezaji wenye uzoefu zaidi, suala hilo liangaliwe kwani hata wakifanya makosa wanajua kujisahihisha mapema tofauti na wanaojaribiwa,” alisema.

Kocha wa zamani wa Stars, Charles Mkwasa alisema bado nafasi ipo ila muunganiko unahitajika katika kikosi ili wachezaji wacheze kwa kuelewena zaidi.

Alisema mashindano makubwa yanahitaji kuwa na wachezaji wenye uzoefu kwa kuwa wanacheza kwa kujiamini zaidi na ambao wanapata nafasi kwa mara ya kwanza wanaweza kujifunza kutoka kwa wenzao na sio kujaribiwa kwani ni kuwabebesha mzigo mzito.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Stars, Ally Mayay alisema kinachohitajika michezo ijayo Tanzania inapaswa kushinda michezo yote miwili ili iweze kufuzu.

Alisema mashindano makubwa kama hayo siku zote yanakuwa kama fainali hivyo hayapaswi kujaribiwa na kuhimiza umuhimu wa Kocha wa Stars kuendelea kufuatilia viwango vya wachezaji ili kuchagua wanaostahili na wenye uzoefu na mashindano makubwa.

Alisema kwa wachezaji wenye vipaji na wanaoitwa kwa mara ya kwanza wanapaswa kujaribiwa katika mechi nyingine za kimataifa kabla ya kupewa nafasi katika michuano hiyo.

Golikipa wa zamani wa Simba, Moses Mkandawile alisema njia pekee itakayowafanya Stars kufuzu ni jitihada na kuwataka wachezaji wajitume kuipigania timu kwa moyo wao wote.

Stars baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia na kufikisha pointi nne Kundi J, ina kazi ya kuhakikisha inashinda michezo miwili ijayo dhidi ya Libya na Guinea ya Ikweta, wakati Tunisia tayari imefuzu baada ya kujikusanyia pointi 10.

Chanzo: HabariLeo