0

Vigogo Simba wajazana mazoezini

Vigogo Simba wajazana mazoezini

Fri, 6 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

KATIKA kile kinachoonekana ni kuongeza hamasa kwa kikosi chao kinachoivaa Yanga kesho Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, vigogo mbalimbali wa Simba wamejitokeza kwa wingi kwenye mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yanayofanyika leo Ijumaa.

Tofauti na mazoezi ya kujiandaa na mechi nyingine ambapo viongozi wa Simba huwa hawaonekani katika Uwanja wao wa Mo Simba Area uliopo Bunju ambako ndiko hufanyia mazoezi, leo mambo yamekuwa tofauti ambapo idadi kubwa ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, maofisa wa sekretarieti na wanachama maarufu wameonekana uwanjani hapa ambako Simba inafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Yanga kesho.

Jopo hilo la vigogo wa Simba linaongozwa na wajumbe watatu wa bodi hiyo ambao ni Mulamu Ng'hambi, Wakili Hussein Kitta na Mohamed Nassor.

Muda mfupi baada ya kikosi cha Simba kuwasili uwanjani hapa, Ng'hambi na Kitta nao waliingia wakiwa kwenye gari aina ya Toyota VX ambapo walikaa humo kwa muda kisha kushuka na kuelekea mahali iliko ofisi ya ufundi na chumba cha kubadilishia nguo ambako walikaa nje kutazama mazoezi hayo.

Wajumbe hao wawili walikuwa wameambatana na aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, Iddi Kajuna na walionekana kuwa na mazungumzo marefu baina yao.

Baadaye mjumbe mwingine wa bodi hiyo Mohamed Nassor aliingia uwanjani hapo akiwa na gari lake aina ya Toyota Harrier.

Chanzo: Mwanaspoti