0

Undule kusaka rekodi Jumapili

Thu, 10 Sep 2020 Source: habarileo.co.tz

BONDIA anayekuja kwa kasi kwenye ngumi za kulipwa nchini, Undule Langson, anatarajiwa kupanda ulingoni Jumapili ijayo katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, kupambana na bondia, Haji Ismail.

Bondia huyo awali alikuwa akishiriki ngumi za ridhaa tangu mwaka 1999 kabla ya mwaka jana kuingia katika ngumi za kulipwa, atapanda kwenye pambano hilo lisilo na ubingwa likiwa ni maalumu kwa ajili ya kutengeneza rekodi.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Undule alisema tayari amefanya maandalizi ya kutosha na ana amini ataibuka na ushindi.

Alisema kama alivyofanya makubwa kwenye ngumi za ridhaa ikiwamo kuiwakilisha nchi kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa, ndivyo atakavyofanya makubwa katika ngumi za kulipwa.

“Pambano hilo la Jumapili litakuwa ni la pili, nilipigana moja nikashinda, natakiwa nipigane mengine ndipo nianze kucheza na mabondia wa kimataifa, nikitoka hili nitapigana lingine Novemba na Januari mwakani.”

“Maandalizi yamekamilika kwa sasa nipo kambini Dar es Salaam, nataka nikienda Morogoro nishinde pambano,” alisema Undule.

Alisema hana uzoefu kwenye ngumi za kulipwa, hivyo ametakiwa kucheza mapambano ya kutafuta rekodi na tayari amecheza moja na amebakiza matatu.

Chanzo: habarileo.co.tz