0

U-17 yapania kombe Cosafa

U-17 yapania kombe Cosafa

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

MORALI ya mchezo wa fainali ya wachezaji wa timu ya wanawake ya Taifa ya soka ya umri chini ya miaka 17 katika mashindano ya Cosafa inayotarajiwa kuchezwa kesho kutwa kwenye Uwanja wa Wolfson, Port Elizabeth nchini hapa imepanda maradufu baada ya kuahidiwa dola za Marekani 15,000 na Kamati ya Saidia Taifa.

U-17 inayofundishwa na kocha Edna Lema imefuzu fainali baada ya kuifunga Comoro 5-1, Afrika Kusini 6-1 na Zimbabwe 10-1 na kufungwa mchezo mmoja na Zambia kwa 2-1 ambao ndio watakaocheza nao fainali.

Akizungumza jana, nahodha wa timu hiyo, Irene Kisisa alisema wamejiandaa vizuri na waamini watarudi nyumbani na kombe.

“Zambia hawawezi kutufunga mara mbili, lazima tutalipa kisasi. Tunazitaka dola 15,000 na hata kama tusingeahidiwa tulipanga kuwafuta machozi dada zetu Twiga Stars,'" alisema Irene.

Naye kocha, Edna alisema wachezaji wana morali na wamefanya mazoezi tangu juzi na hakuna majeruhi.

"Kumfunga Zambia ni muhimu na wachezaji wana ari wanataka kulipa kisasi na wamesema watarudi na kombe," alisema Edna.

Mashindano ya Cosafa yanahusisha timu 10 za taifa za wakubwa za wanawake na sita za wasichana U-17 yanatarajiwa kumalizika kesho Jumamosi.

Chanzo: HabariLeo