0

Twiga Stars yajiweka pagumu Cosafa

Twiga Stars yajiweka pagumu Cosafa

Sun, 8 Nov 2020 Source: HabariLeo

TIMU ya soka ya taifa ya wanawake Twiga Stars, imefungwa na Botswana kwa bao 1-0 katika mchezo wa michuano ya Cosafa, uliochezwa kwenye Uwanja wa Wolfson, Port Elizabeth, Afrika Kusini jana.

Huu ni mchezo wa pili kwa Twiga Stars baada ya ule wa awali kuifunga Zimbabwe kwa bao 1-0 lililofungwa na Amina Shekigenda dakika ya 60.

Twiga Stars ambayo inafundishwa na kocha Bakari Shime inaongoza Kundi C ikiwa na pointi tatu sawa na Botswana lakini imebakisha mchezo mmoja dhidi ya Zimbabwe.

Kwa matokeo hayo matarajio ya Twiga ya kusonga mbele yapo kwenye ‘best loser’ ili kufuzu nusu fainali.

Kundi A wenyeji Afrika Kusini inaongoza ikiwa na pointi sita baada ya kuifunga Angola na eSwatini na Angola ina pointi tatu baada ya kuifunga eSwatini.

Kundi B Zambia inaongoza kwa pointi tatu baada ya kuifunga Lesotho na Malawi jana jioni ilitarajiwa kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Lesotho.

Wakati huo huo timu ya soka ya wanawake ya Taifa ya umri chini ya miaka 17, Tanzanite inatarajiwa kucheza mchezo wa tatu wa michuano hiyo dhidi ya wenyeji Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Oval mjini Port Elizabeth leo.

U17 ambayo ina pointi tatu inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kucheza fainali japo wanacheza kwa mtindo wa ligi lakini baada ya kila mmoja kucheza michezo minne timu za juu zitacheza mchezo mmoja kutafuta bingwa

Zambia inaongoza baada ya kushinda michezo yake miwili ikifuatiwa na Afrika Kusini ambayo juzi iliifunga Comoro kwa mabao 7-0

Akizungumza baada ya mazoezi yalifanyika jana kocha wa U17, Edna Lema alisema mchezo wa leo ni muhimu kushinda ili wacheze fainali.

"Wachezaji wanajua umuhimu wa mchezo wa kesho (leo) hivyo wameniahidi kufanya vizuri japo mchezo utakuwa mgumu lakini aliyejiandaa vizuri atashinda," alisema Edna.

Alisema kikosi chake kipo imara na hakina majeruhi na kwa ari waliyokuwa nayo mazoezini anaamini watashinda.

Michuano hii inahusisha pia timu 10 za wakubwa na tano za wasichana U17 yanatarajiwa kumalizika Novemba 14.

Chanzo: HabariLeo