0

Tume yabaini upungufu rekodi za mabondia

Tume yabaini upungufu rekodi za mabondia

Wed, 18 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By Imani MakongoroDar es Salaam. Tume iliyoundwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kufuatilia kufutwa matokeo ya mapambano yaliyochezwa nchini kuanzia 2018 hadi sasa, imeeleza kubaini upungufu.

Hivi karibuni mtandao wa dunia wa ngumi za kulipwa (Boxrec) ulifuta matokeo ya mapambano yote yaliyochezwa tangu 2018, huku kaimu rais wa TPBRC, Agapeter Basil ‘Mnazareth’ akidai kuna hujuma kwenye hilo.

Agapeter aliunda tume kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kufutwa na kueleza kuwa itafanya kazi kwa siku saba ambazo zilimalizika juzi.

Jana, mwenyekiti wa tume hiyo, Juma Ndambile aliliambia gazeti hili kwamba wamebaini upungufu mwingi katika upelekaji Boxrec wa matokeo ya mapambano yanayochezwa hapa nchini.

“Tumekamilisha kazi yetu, ila kuna upungufu mwingi ambao tumeubaini katika utaratibu mzima wa upelekaji matokeo Boxrec, tutapeleka ripoti TPBRC na wao ndio watajua ni hatua gani wachukue katika hilo,” alisema.

Agapeter alipoulizwa juu ya hatua za kuchukua baada ya ripoti ya tume, alisema atahakikisha rekodi za mabondia wa Tanzania zinarejeshwa kama ilivyokuwa awali.

Chanzo: Mwanaspoti