0

Taifa Stars waanza maandalizi makali Uturuki

Taifa Stars waanza maandalizi makali Uturuki

Tue, 10 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By Oliver Albert Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanya mazoezi yake ya kwanza jana nchini Uturuki ilikoweka kambi kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Tunisia

Stars iliyopo Kundi J itaikabili Tunisia Novemba 13 kwenye Uwanja wa Stade Olympique de Rades, mjini Tunis, na timu hizo zitarudiana Novemba 17 jijini Dar es Salaam.

Stars itaweka kambi ya siku tatu nchini Uturuki kisha itaeleka Tunisia na tayari baadhi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamejiunga na timu hiyo akiwemo Himid Mao anayecheza Misri.

Taifa Stars haina budi kupambana ili kushinda mchezo huo ili kujiwekea matumaini ya kufuzu kwa fainali hizo baada ya mchezo uliopita kulala kwa mabao 2-1 dhidi ya Libya, mchezo uliofanyika Novemba 20, mwaka jana.

Awali Stars ilianza mashindano hayo vizuri kwa kuifunga Equatorial Guinea bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Novemba 15 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkapa. Bao la ushindi lilifungwa na Salum Abubakary ‘Sure Boy’.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi Taifa Stars kuikabili Tunisia na inatakiwa kujipanga wapinzani wao kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka barani Ulaya.

Chanzo: Mwanaspoti