0

Taifa Stars hakuna kulala

Taifa Stars hakuna kulala

Mon, 16 Nov 2020 Source: HabariLeo

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imerejea nchini na kuanza mazoezi kwa ajili ya kurudiana na Tunisia katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2021) utakaofanyika kesho Dar es Salaam.

Taifa Stars yenye pointi tatu katika Kundi J, inarudiana na Tunisia ambao wanaoongoza kundi hilo, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya Ijumaa kufungwa 1-0 ugenini.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda jana alisema Taifa Stars waliwasili salama jana asubuhi na moja kwa moja waliingia kambini jijijni Dar es Salaam na jioni walianza mazoezi kujiandaa na mchezo wa kesho.

Alisema wachezaji wote wako vizuri isipokuwa nahodha wao, Mbwana Samatta ambaye alikosa mchezo wa mwanzo nchini Tunisia kutokana na majeruhi.

Stars ina pointi tatu baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Guinea ya Ikweta 2-1, kabla ya kupoteza dhidi ya Libya 2-1 na Tunisia 1-0 na hivyo inahitaji ushindi kesho kurejesha matumaini ya kufanya vizuri.

Tanzania imecheza mara mbili fainali za Afcon mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 Misri na sasa inasaka kucheza kwa mara ya tatu fainali hizo ambazo mwakani zitapigwa Cameroon. Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alisema juzi kuwa wameyaona makosa waliyofanya wakati wa mchezo wa Tunisia, hivyo watayafanyia kazi kuhakikisha hawayarudii tena.

Chanzo: HabariLeo