0

Sven hesabu kali kwa Yanga, Azam

Sven hesabu kali kwa Yanga, Azam

Fri, 6 Nov 2020 Source: HabariLeo

KOCHA wa Simba, Sven Vandebrock anazipigia hesabu kali mechi za Yanga na Azam FC namna ya kufanya vizuri dhidi yao ili kurahisha mipango ya kutetea taji la Ligi Kuu.

Simba baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi kwenye Uwanja wa Uhuru imewasogelea wapinzani wake Azam na Yanga kwa tofauti ndogo ya pointi.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Sven alisema iwapo watashinda mechi mbili za Yanga na Azam FC njia itakuwa nyeupe kwao kuwa mabingwa.

“Kushinda kila kitu ni ngumu sasa tumebakiza pointi chache kulingana nao, tuna kila kitu mikononi mwetu muhimu ni kushinda mechi mbili za Yanga na Azam hapo sasa ubingwa unaweza kuwa karibu yetu,” alisema.

Kocha huyo alisema kuna muda ni ngumu kushinda kila kitu na wao malengo sio kuwatazama Yanga tu, bali ni kufanya vizuri michezo yao yote iliyoko mbele yao.

Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajiwa kukutana na watani wao wa jadi Yanga katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu utakaochezwa kesho.

Alisema kuelekea katika mchezo huo anawahofia wachezaji wake Shomari Kapombe na Cletus Chama ambao licha ya kucheza dhidi ya Kagera Sugar walionekana hawako vizuri wakichechemea hatua iliyowalazimu kutolewa kabla ya kumalizika kwa mchezo huo.

Alisema anaendelea kuwatazama wachezaji hao katika mazoezi akiwa na imani watakuwepo katika mchezo ujao dhidi ya Yanga.

Sven alisema iwapo atawakosa itakuwa pigo kwani anatamani wachezaji wote wazuri wawepo.

“Unaweza kuchagua wachezaji waliopo lakini kuna muda unatamani kuchagua wale wazuri wacheze ingawa huwezi kumtegemea kila mtu kwa asilimia 100 awe mzima kila siku,” alisema.

Kuhusu mchezo uliopita, alisema alifurahishwa na kiwango kizuri kipindi cha kwanza ila cha pili walijaribu kuua mchezo hadi dakika 90.

"Malengo yetu ni kutetea ubingwa lakini lazima tupambane kutafuta matokeo mazuri kwa kila mechi zetu bila kujali tunacheza na timu gani, wachezaji wangu wanajua hilo na kila ninayempa nafasi anaonyesha kiwango kizuri."

"Leo (juzi) nimewapa nafasi wachezaji ambao wametoka katika majeruhi Chris Mugalu na Ame Ibrahim na wamefanya kazi nzuri," alisema Sven.

Alisema baada ya mechi ya juzi dhidi ya Kagera Sugar waliyoshinda mabao 2-0 anafanya maandalizi ya kuikabili Yanga hapo kesho.

"Tunaenda kujipanga kwa mechi zetu zijazo hivi sasa tunajiandaa dhidi ya Yanga kwa kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita," alisema Sven.

Kuhusu Mugalu alisema amerejea kikosini baada kupona majeraha ya nyoga na ana imani mechi ijayo atakuwa miongoni mwa watakaokuwepo katika mipango yake.

"Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa daktari wetu wa timu, tutawakosa wachezaji wawili Meddie Kagere na Gerson Fraga ambao wana majeraha ya muda mrefu," alisema kocha huyo.

Alisema malengo yake ni kuona timu hiyo inarejea katika nafasi ya juu ikiongoza ligi kabla ya kwenda kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi ya kesho, Simba itakuwa ugenini ikitarajiwa kuwa mechi ngumu kutokana na ugumu wa timu hizo zinapokutana.

Simba bingwa mtetezi ikiwa kwenye kiwango bora msimu uliopita, ilishindwa kuifunga Yanga katika mechi zote mbili za Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mechi ya kwanza kabla ya kufungwa bao 1-0 katika mechi ya pili.

Chanzo: HabariLeo