0

Sven aifikiria Biashara

Sven aifikiria Biashara

Mon, 14 Sep 2020 Source: HabariLeo

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kwa sasa anakiandaa kikosi chake kujipanga na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kucheza kwenye uwanja wa nyumbani, baada ya mechi mbili za mwanzo kuzipiga ugenini dhidi ya Ihefu ya Mbeya na kushinda 2-1 na Mtibwa Morogoro na kutoka sare ya 1-1.

Sven ametoa kauli hiyo siku moja baada ya kikosi cha Simba kuambulia pointi moja kwenye mchezo wa pili wa ligi hiyo kufuatia sare na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Kocha huyo alisema sio wakati wa kujadili matokeo ya mchezo uliopita bali wamepokea kama changamoto ya kujipanga kwa mchezo ujao, ambao utakuwa fainali ya kusaka ushindi utakao warudisha kwenye mstari.

“Hii ni ligi bado tuna mechi nyingi mbeleni, sio wakati wa kukaa na kujuta tulichopata ila tumepokea kama changamoto kuona tunatengeneza mbinu mpya kujipanga na mechi ijayo dhidi ya Biashara,” alisema Sven, raia wa Ubelgiji.

Alisema msimu unapoanza kila timu inakua na kauli mbio ya kufanya vema kutengeneza msingi wa saikolojia ya ushindi kujipanga na mechi zilizo mbele yao, hivyo wao kama mabingwa watetezi bado wanatakiwa kuendelea kujipanga.

Aidha, Sven amezungumzia changamoto ya uwanja kuwa ni sababu iliyochangia kikosi chake kupata matokeo hayo, ambayo sio mabaya, lakini yanawapa picha ya kujipanga kiushindani kwenye kila mchezo unaokuja ili kupata ushindi na kutimiza malengo waliyojiwekea.

Kwa upande wake, kocha wa Mtibwa Sugar Zuber Katwila, alisema usajili wa wachezaji nane ni sababu iliyofanya kikosi chake kuonesha ushindani mkali dhidi Simba na kupata pointi moja inayowafanya kuanza kujipanga kwa mechi ijayo.

“Tulifanya usajili mkubwa, lengo letu lilikuwa ni kuonesha ushindani kwa kufanya vizuri kwenye ligi na tusirudie yaliyokuta msimu uliopita,” alisema Katwila.

Matokeo hayo yamewafanya Simba kufikisha pointi nne na kushuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo, huku wapinzani wao Mtibwa Sugar wako nafasi ya nane wakiwa na pointi mbili baada ya kutoka sare mechi zake mbili.

Wakati huohuo, Ihefu FC jana ilijikusanyia pointi tatu muhimu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokone, jijini Mbeya.

Aidha, Ligi Kuu itaendelea tena leo kwa Namungo FC kuwa wenyeji wa Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa, Lindi.

Chanzo: HabariLeo