0

Stars yaelekeza matumaini Dar

Stars yaelekeza matumaini Dar

Sat, 14 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By RAMADHAN ELIASBaada ya jana Novemba 13 timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kupoteza mchezo wa raundi ya tatu kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afika 2021 (AFCON) dhidi ya Tunisia ugenini kwa kufungwa bao 1-0, timu hiyo inatarajia kurejea Bongo kujiandaa na mchezo wa marudiano utakaopigwa Novemba 17.

Bao pekee la mkwaju wa penati walilofunga Tunisia dakika ya 18, baada ya golikipa wa Stars Aishi Manula kumchezea madhambi nyota na nahodha wa timu hiyo Youssef Msakni lilitosha kuwapa ushindi Tunisia kwenye mechi hiyo.

Licha ya Kocha mkuu wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa kuwaanzisha Aishi Manula, Erasto Nyoni, Himid Mao, Farid Mussa na John Bocco ambao hawakuanza kwenye mchezo wa mwisho wa timu hiyo iliocheza dhidi ya Burundi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 11 mwaka huu, lakini walishindwa kufurukuta mbele ya Tunisia.

Taifa Stars ipo Kundi J kwenye hatua ya makundi kuwania kufuzu fainali hizo ikiwa na timu nyingine tatu za Libya, Equatorial Guinea na Tunisia ambapo zinahitajika timu mbili pekee kutoka kundi hilo zitakazofuzu kucheza michuano hiyo itakayo fanyika nchini Cameroon mwakani.

Mchezo unaofuata utakua wa marudiao dhidi ya Tunisia unaotarajiwa kuchezwa Jumanne ya Novemba 17, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo Stars watakuwa wenyeji.

Mpaka sasa Taifa Stars wanashika mkia kwenye kundi hilo linaloongozwa na Tunisia wenye alama tisa baada ya kushinda michezo yote mitatu ya awali huku Equatorial Guinnea, Libya na Tanzania wote wakiwa na alama sawa (tatu) baada ya kushinda mechi moja na kupoteza mbili kwa kila mmoja tofauti ikiwa ni idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Chanzo: Mwanaspoti