0

Stars kufa au kupona Tunisia

Stars kufa au kupona Tunisia

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

TIMU ya Taifa ya Soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo itashuka dimbani ugenini dhidi ya wenyeji Tunisia katika mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2021).

Mchezo huo ni muhimu kwa Stars kupata matokeo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu.

Tunisia ndio kinara wa Kundi J baada ya kushinda michezo miwili iliyopita dhidi ya Libya mabao 4-1 na dhidi ya Guinea ya Ikweta bao 1-0.

Aidha, Stars ilishinda mchezo mmoja uliochezwa awali nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta na kupoteza ugenini dhidi ya Libya kwa mabao 2-1.

Katika kundi hilo kila mmoja ana nafasi, ambapo Tunisia ina pointi sita, wengine wote kila moja ina pointi tatu hivyo nani ana nafasi itategemea na matokeo ya mechi zao zijazo.

Katika mchezo wa leo Stars itamkosa nahodha wake, Mbwana Samatta aliyeumia katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Uturuki kati ya Fenerbahce na Konyaspor waliofungwa mabao 2-0.

Lakini Stars ina wachezaji wengine wazuri wakiongozwa na mshambuliaji Simon Msuva, John Bocco na wengine ambao asilimia kubwa ni wale wanaocheza Ligi Kuu soka Tanzania.

Wapinzani wao Tunisia wana kikosi chenye wachezaji wanaocheza soka la kulipwa klabu mbalimbali za Afrika na Ulaya na baadhi yao kutoka ligi ya nyumbani kwao.

Ushindi wa kila mmoja utategemea na maandalizi mazuri yaliyofanywa kwa ajili ya mchezo huo kwa kutizama ubora na udhaifu wao.

Stars awali iliweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na mchezo huo kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji vizuri katika mazingira yaliyotulia.

Kocha Mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije alisema kikosi chake kimefanya maandalizi mazuri na ana imani watafanya kile alichowaelekeza.

Alisema licha ya kuwa Samatta atakosekana katika mchezo huo hilo halimpi presha akiamini waliopo wataipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Tumefanya maandalizi mazuri na kila mmoja ameonesha morali ya hali ya juu.

Tunajua mchezo utakuwa mgumu kwasababu Tunisia ni timu nzuri lakini matokeo yanapatikana uwanjani, tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema.

Msuva aliwaomba Watanzania kuwaombea akisema mchezo huo hautakuwa rahisi ila wamejipanga na wako tayari kwa mapambano.

Chanzo: HabariLeo